Somo la 8: Kupanga kwa Ajili ya Mafanikio

Mithali 3, Mathayo 33
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
8

Somo la 8: Kupanga kwa Ajili ya Mafanikio

(Mithali 3, Mathayo 33)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mojawapo ya baraka kubwa maishani mwangu ni kwamba ninayo fursa ya kuwasaidia wanafunzi wa sheria kupangilia mipango yao ya baadaye. Hivi karibuni, mwanafunzi mmoja aliniambia kuwa lengo lake ni kupata fedha. Aliutafakari mfano wa Mkuu wa shule yetu ya sheria. Mkuu huyu alikuwa mmiliki mwenza katika mojawapo ya kampuni kubwa za sheria nchini Marekani. Baada ya miongo kadhaa alijipunguzia mshahara kwa kiasi kikubwa sana na kuanza kufundisha katika shule ya sheria ya Kikristo, mahala ambapo ninafundisha. Nilimwambia mwanafunzi yule kwamba kwanza kujiingizia fedha husababisha tatizo gumu la kushindwa kugeuka nyuma na kuziacha fedha hizo. Kama mbadala wa hilo nilimwelezea mpango wa maisha yangu – tangu mwanzo kabisa lengo langu lilikuwa ni kumfanyia Mungu kazi. Ingawa mara zote nimekuwa nikifanya kazi kwenye shirika lisilo la kiserikali lisilopata faida, Mungu amenibariki kwa kila namna. Wewe unayachukuliaje mafanikio? Maisha ya utulivu? Familia yenye upendo? Kazi unayoifurahia? Fedha? Nyumba nzuri? Magari mazuri? Kusafiri duniani kote? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuchimbue kanuni ya mafanikio!

I.  Maisha ya Utulivu

A.  Soma Mithali 3:1-2. Lengo la amri ni nini? (Kuzishika amri hukupatia “amani,” “wingi wa siku,” na “miaka ya uzima.”)

1.  Baraka hizi tatu kwa Kiebrania ni orech yamim (wingi wa siku), shenoth chaiyim (miaka ya uzima) na shalom (usitawi). Je, huu ndio msingi ya maisha yenye mafanikio?

2.  Unauelewaje “wingi wa siku?” Je, inamaanisha siku ndefu ya kazi? Kazi hiyo ni ngumu na yenye uchoshi? (Ni mara ngapi umesema, “Ninatamani kungekuwa na saa nyingi zaidi katika siku?” Nadhani hapa ahadi ni kwamba una uwezo wa kutimiza mambo unayotaka kuyakamilisha katika siku moja.)

B.  Soma Mithali 3:3-4. Tunapaswa “kufunga” nini shingoni mwetu? Ninadhani “kufunga” maana yake ni kuziwazia kila mara. (Upendo imara na uaminifu.)

1.  Ni nini maana ya upendo imara na uaminifu? (Kuwa mpole na mwaminifu kwa wengine.)

2.  Matokeo ya kufanya hivyo ni yepi? (Mungu na wanadamu watakuonesha upendeleo na kukusaidia kupata mafanikio.)

C.  Soma Mithali 3:5-7. Inamaanisha nini “kuzitegemea” akili zako mwenyewe na kuwa mwenye “hekima” machoni pako? (Tunatakiwa kufuata ushauri wa Mungu badala ya kufuata mawazo yetu wenyewe kuhusu jinsi ya kupata mafanikio.)

1.  Inamaanisha nini kumtumaini Mungu badala ya kujitegemea mwenyewe? (Mpe Mungu sifa badala ya kujisifia mwenyewe.)

2.  Kujiepusha na uovu inaonekana kuwa jambo la wazi. “Mapito yaliyonyooka” ni kitu gani? (Katika mazoezi yangu huwa ninaendesha baiskeli ya miguu mitatu ambayo uendeshaji wake mgongo wangu unakuwa kama umelala. Huwa ninaendesha kwenye barabara ya lami iliyonyooka na tambarare. Hiyo inanifanya niendeshe kwa kasi. Njia nyoofu ndio njia ya haraka kusonga mbele.)

D.  Jordan Peterson anatoa ushauri mzuri kuhusu maisha. Anasema kuwa tunapaswa kuyakumbatia magumu kwa sababu yanatusaidia kukua. Soma Mithali 3:11-12. Hii inatufundisha nini kuhusu utulivu? (Matatizo na ukosoaji hutufundisha kwa njia bora. Hiyo ndio njia kuu ya kuufikia utulivu.)

1.  Je, haya ndio mambo ambayo tumeyajadili kwamba yanahusika katika kuwa na maisha ya kifamilia yenye utulivu?

II.  Mafanikio ya Mali

A.  Soma Mithali 3:9-10. Utakumbuka kwamba huwa nina huu mjadala endelevu na kikosi changu cha Shule ya Sabato kuhusu kama msingi mkuu wa Malaki 3 unahusu fedha au aina nyingine za baraka. Aina gani ya baraka inaahidiwa hapa? (Mali. Ghala iliyojaa na mashinikizo yaliyofurika inamaanisha kuwa ulikuwa na mafanikio ya mali.)

1.  Jambo gani linahitajika? (Kwamba unampa Mungu “mazao ya kwanza,” kwamba unamheshimu kwa mali yako.)

B.  Soma Mhubiri 12:1. Unakumbuka katika sehemu ya utangulizi nilipozungumzia njia ya Mkuu wa shule ya sheria maishani dhidi ya mpango wangu? Hii inaegemea upande gani? (Inaegemea upande wa kumtanguliza Mungu tangu mwanzo kabisa kwa sababu nilizozipendekeza – ni vigumu kubadili uelekeo baadaye maishani. Hata hivyo, Mungu anawahitaji watu wake katika matabaka yote ya jamii. Kusingekuwa na ubaya wowote kwa Mkuu wa shule ya sheria kusalia katika kampuni mashuhuri ya sheria na kuwa shuhuda wa Kristo.

1.  Tatizo kubwa la wanasheria wa Kimarekani ni kwamba baada ya muongo mmoja au miwili hawaifurahii kazi yao. Bila shaka ukweli huu pia unahusika kwenye taaluma nyingine. Je, hicho ndicho kinachomaanishwa kwenye “Mimi sina furaha katika hiyo?” (Hilo ni hitimisho moja lenye mantiki. Kutafuta fedha ni changamoto ya kila siku. Inaweza isiwe ya kufurahisha sana.)

C.  Soma tena Mithali 3:3. Kama una kazi ambayo unawasaidia wengine, je, kazi hiyo inaweza kukuchosha? (Kama wale unaowasaidia wana shukurani kamwe hutaichoka kazi yako.)

D.  Soma Mathayo 6:33. Ni nini kanuni ya Mungu kwa ajili ya mafanikio na maisha ya utulivu? (Utafute kwanza Ufalme wa Mungu.)

1.  Hilo litaonekanaje kivitendo? (Kuutangaza Ufalme wa Mungu kuna kipaumbele. Hicho kitakuwa kipaumbele cha muda na kipaumbele cha umuhimu. Kama unafundisha somo hili, itamaanisha kulipa kipaumbele cha kwanza wakati wa asubuhi. Itamaanisha kwamba huruhusu majukumu mengine yafanye uliweke somo hilo kuwa jambo la mwisho katika siku zako za juma.)

III.  Kazi

A.  Soma Mwanzo 2:15. Kwenye bustani kamilifu, kwa nini wanadamu wahitajike kufanya kazi?

1.  Kati ya kazi zote ambazo wangeweza kuzifanya, kwa nini Mungu achague bustani?

B.  Soma Mwanzo 3:17-19. Je, kazi sio rafiki yetu tena? Je, uhusiano wetu na kazi umebadilika sana tangu Bustani ya Edeni?

1.  Ni jambo gani hasa limetokea kwenye kazi? (Imekuwa ngumu zaidi. Juhudi za kuzalisha chakula zimeongezeka zaidi.)

2.  Kwa nini Mungu alifanya hivyo? Je, ni adhabu stahiki? Kisasi? Au jambo jingine? (Kura yangu inaangukia kwenye jambo jingine. Kwanza, ni ukumbusho kwamba kuzishika amri za Mungu huyarahisisha maisha yako. Pili, tunajifunza kutokana na changamoto, na kwa dhahiri wanadamu walihitajika kujifunza zaidi.)

C.  Soma Kumbukumbu la Torati 31:6-7. Ukitaka kumiliki kitu fulani, nini kinahitajika? (Kuwa “hodari na moyo wa ushujaa.”)

1.  Je, changamoto zitakufanya uwe hodari na moyo wa ushujaa? (Kazi zina changamoto hivyo inatusaidia kuwa “hodari na moyo wa ushujaa.”)

2.  Baba yangu alipokuwa mdogo, alipitia kipindi cha “Great Depression” kisha akajikuta akiwa sehemu ya uvamizi wa Normandy. Alijeruhiwa mara tatu na alikuwa katika eneo la vita kwa muda wa miezi 33. Baadhi ya vijana wa leo ni wadhaifu sana kiasi kwamba hawawezi kusikiliza hoja kinzani. Tunawasaidiaje wanaume dhaifu na waoga? (Suluhisho lililopendekezwa katika kitabu cha Mwanzo 3 ni juhudi ya kazi.)

D.  Soma 1 Wakorintho 10:31 na Wakolosai 3:23-24. Tunapaswa kufanyaje kazi? Tunapaswa kufanya kazi kwa namna inayoakisi utukufu kwa Mungu. Tunaichukulia kazi yetu kama kumfanyia Mungu kazi, sio kuwafanyia wanadamu. Tunautafuta ubora.)

1.  Je, ungependa mtu mwenye mtazamo huo akufanyie kazi?

2.  Kama wewe ni mfanyakazi mwenye mtazamo huu, je, kuna uwezekano ukakabiliana na tatizo la uhuru wa dini kazini kwako? (Mara kwa mara huwa ninatumia sheria kulinda uhuru wa dini wa waajiriwa katika maeneo ya kazi. Hata hivyo, ninashawishika kuamini kwamba katika eneo dogo la kazi (ambapo wamiliki wanakufahamu) ulinzi mzuri wa imani yako ni kuwa mfanyakazi ambaye mwajiri wako asingependa kumpoteza.)

E.  Soma Mithali 16:2-3. Je, tunaweza kujidanganya wenyewe kuhusu nia zetu kazini? (Hii inaashiria kwamba hatuwezi kujitumaini wenyewe.)

1.  Tunaepukaje tatizo hili? (Kwa kuikabidhi kazi yetu kwa Mungu.)

F.  Soma Mithali 16:7. Je, umewahi kuwasikia watu wakidai kwamba sababu ya wao kuwa na matatizo kazini kwao ni kutokana na imani za dini? Wanasema kwamba kama wewe ni Mkristo mzuri, wewe pia utapata masumbufu kazini kwako. Kuna fundisho gani katika kifungu hiki? (Kinathibitisha kwamba tutakuwa na maadui. Lakini kama wewe ni mtendakazi mzuri ambaye unampendeza Mungu, atashughulika na vizingiti vinavyokukabili kazini kwako.)

G.  Rafiki, je, unapenda kufanikiwa maishani? Mtangulize Mungu. Hiyo maana yake ni kwamba tii amri alizozitengeneza kwa manufaa yako. Inamaanisha kwamba kipaumbele cha fedha zako na muda wako ni kuutangaza ufalme wa Mungu. Inamaanisha kuziangalia changamoto na ukosoaji kama njia ya kuwa bora zaidi. Kwa nini usifanye uamuzi sasa hivi, kufuata njia ya Mungu kwa ajili ya kupata mafanikio?

IV.  Juma lijalo: Jilindeni na Choyo.