Somo la 7: Kwa Mmojawapo wa Hao Walio Wadogo

1 Timotheo 5, Mambo ya Walawi 19, Luka 19
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Somo la 7: Kwa Mmojawapo wa Hao Walio Wadogo

(1 Timotheo 5, Mambo ya Walawi 19, Luka 19)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mwanzoni nilipoanza kuendesha gari ilikuwa ni nadra sana kuwabeba watu wanaoomba lifti barabarani nisiowafahamu. Siku moja asubuhi katika majira ya kiangazi nilikuwa kwenye gari na kaka yangu tukielekea kwenye kazi ya ujenzi wakati gari lake zuri lakini lisilo la kuaminika lilipoharibika. Ghafla, niliyaona mambo kwa upande mwingine pale nilipohitaji kutumia gari! Mojawapo ya changamoto ninayoipata katika kuandika somo hili ni kwamba nina wasiwasi kwamba nina upendeleo kutokana na kutokuwa na uzoefu na hivyo kutowahurumia maskini. Ni pale tu nilipooa ndipo nilikuwa maskini. Changamoto nyingine kubwa ni kwamba watu maskini waliopo nchini Marekani na katika nchi nyingine za kidemokrasia wana mazingira tofauti sana kuliko watu maskini waliopata kutokea katika historia ya dunia. Katika nchi ya kidemokrasia watu maskini wanaweza kupiga kura kwa wingi na wanawazidi matajiri. Maskini wanajipigia kura ya kupata fedha na manufaa mengineyo ambayo yanachukuliwa kutoka kwa matajiri bila kupenda kwao. Matokeo yake ni kwamba, wote, yaani matajiri na maskini, wanajisikia kutendewa haki. Nchini Marekani, asilimia kubwa ya watu hutoa sehemu yao ndogo ya fedha kuwasaidia wengine kwa sababu kundi hili limeridhika na kupiga kura kuhusu kugawanya fedha kutoka kwa matajiri kwenda kwa maskini. Biblia inatufundisha nini kuhusu mazingira kama hayo? Inamaanisha nini kuwa na mtazamo kama aliokuwa nao Yesu kwa maskini katika muktadha wa jamii kama yetu? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

I.  Miongoni Mwa Hao Wadogo

A.  Soma Zaburi 68:5 na Isaya 1:17. Vifungu hivi viwili vinaashiria nini kuhusu wajane na yatima?

B.  Soma Kumbukumbu la Torati 14:28-29. Hii inazungumzia nini kuhusu zaka na kuwategemeza wajane na yatima? (Katika mwaka wa tatu zaka ilipelekwa mjini na sehemu yake kutumika kuwalisha wajane na yatima.)

C.  Soma Yakobo 1:27. Yakobo anasema nini kuhusu kuwasaidia wajane na yatima? (Biblia haibadiliki katika kuwaelezea wajane na yatima kama watu wanaohitaji msaada zaidi. Kweli watakuwa “miongoni mwa walio wadogo.”)

II.  Paulo na Miongoni Mwa Walio Wadogo

A.  Soma 1 Timotheo 5:3-5. Paulo anamaanisha nini anapoandika kuhusu kuwaheshimu wajane “walio wajane kweli kweli?” Je, anadhani kuwa wana mume waliyemficha mahala? (Hapana. Paulo anafafanua “mjane” kumaanisha mwanamke mzee ambaye kweli ameachwa peke yake. Hana familia ya kumsaidia. Kama ana familia, basi wanafamilia wanapaswa kumsaidia.

B.  Soma 1 Timotheo 5:8. Amri gani imetolewa juu ya kuwasaidia wanafamilia? (Wanafamilia wanalazimika kuwasaidia ndugu. Hiki kinapaswa kuwa kipaumbele kwa familia.)

C.  Soma 1 Timotheo 5:16. Nani anayetakiwa kutoa msaada hapa? (“Mwanamke aaminiye” anayehusiana na mjane. Kwa mara nyingine, tunamwona Paulo akiwarejelea wale ambao ni “wajane kweli kweli” kama mwanamke asiye na ndugu anavyoweza kutoa msaada.)

1.  Hebu tuangalie muktadha wa swali la kisasa. Ikiwa katika mfumo wa leo wa masuala ya ustawi wa kijamii, mjane anaweza kuitegemea serikali kumsaidia je, huyo ni “mjane” kweli kwa malengo ya mjadala wa Paulo?

2.  Je, serikali inaziweka huru familia dhidi ya wajibu huu?

D.  Soma 1 Timotheo 5:9 na Matendo 6:1-2. Hapa tunaona mfumo gani? (Inaleta mantiki kuhitimisha kwamba kanisa la awali lilikuwa na mfumo wa ustawi kwa ajili ya wajane. Ni jambo linalofanana na mfumo wetu wa ustawi wa kisasa ambapo wajane “wanaandikishwa.”)

E.  Soma 1 Timotheo 5:9-13. Kigezo cha kuandikishwa ni kipi? (Kuna kigezo cha umri, kigezo cha tabia, na sera inayowakataa wale watakaohamasishwa kutokuwa na kazi (idle).)

1.  Je, hivi ndivyo vigezo tunavyopaswa kuvitumia leo katika programu za ustawi za serikali?

2.  Je, hivi ndivyo vigezo tunavyopaswa kuvitumia katika utoaji wetu wa kuwasaidia miongoni mwa walio wadogo?

III.  Hao Walio Wadogo na Kazi

A.  Soma 2 Wathesalonike 3:10-12. Je, tunapaswa kuwapatia watu fedha kwa kuwa tu wao ni maskini? Au tunapaswa kuwataka maskini wafanye kazi? (Kifungu hiki kinasema kuwa wale wasio radhi kufanya kazi hawapaswi kula.)

1.  Je, huo sio ukatili kwa kiasi fulani? Kwa nini Biblia inaagiza watu kufanya kazi? (Hatupaswi kuwahamasisha watu kutokuwa na kazi (idle) na kuingilia mambo ya watu wengine.)

2.  Je, panapaswa kuwepo na ukomo wa umri kwenye kigezo cha kazi? (Baadhi ya Wakristo wanajenga hoja kwamba kamwe hatupaswi “kustaafu,” lakini sidhani kama hilo linatetewa na Biblia. Makuhani walistaafu kutoka kwenye utumishi katika umri wa miaka 50. Hesabu 8:24-26.)

B.  Soma Ezekieli 16:49. Hii inazungumzia nini juu ya kutofanya kazi? (Uvivu unaweza kuwaambukiza maskini na matajiri. Tatizo la Sodoma halikuwa tu “kufanikiwa,” lakini sio kuwaunga mkono “maskini na wahitaji.”)

1.  Au, tatizo ni kwamba watu walio na “chakula cha ziada” na “waliofanikiwa” hawakuwasaidia maskini? Je, ni kusema tu kwamba walikuwa na muda na chakula kwa ajili ya kutoa msaada, tofauti na kushutumu “mafanikio?”

C.  Soma Mithali 20:13, Mithali 28:19, Mithali 15:19-21, na Mithali 21:25-26. Tufikie hitimisho gani kutokana na vifungu hivi kuhusu kuwa masikini wala kutokuwa wazingativu? (Uzembe una matokeo mabaya.)

1.  Je, tuna wajibu wa Kikristo wa kuhamasisha utendaji kazi na uwekaji malengo miongoni mwa wavivu?

D.  Soma Mambo ya Walawi 19:9-10. Hii ni kanuni ya masazo ya mavuno. Inakusudia kumsaidia nani? (Maskini na msafiri.)

1.  Kama una uzoefu wa ukulima, mazao yaliyopo kwenye pembe ye shamba yanakuaje? (Kwa uzoefu wangu mdogo kabisa, mazao yanakuwa mabaya zaidi kwenye kona ya shamba. Faida ya kanuni hii kwa mkulima ni kwamba mkulima anaweza kujikita kwenye mavuno yake katika maeneo yaliyozaa sana shambani mwake.)

2.  Masazo ya mavuno yanawataka maskini wafanye nini? (Wanatakiwa kufanya kazi. Hawana haja ya kumiliki ardhi au kulima mazao, bali wanatakiwa kwenda na kuvuna au kuokota mazao yaliyoanguka.)

E.  Soma Mambo ya Walawi 19:15. Kuna ubaya gani kumpendelea maskini? (Mungu anataka haki. Haruhusu upendeleo kwa maskini au tajiri.)

IV.  Msaada Usiostahili

A.  Soma Luka 14:12-14. Hii inatufundisha kanuni gani juu ya kuwasaidia maskini? (Huu ni msaada usiostahili. Je, Biblia inatufundisha jambo zaidi ya kuwataka maskini kufanya kazi?

B.  Yesu aliingia Yeriko ambapo mtu Tajiri kwa jina la Zakayo alitaka kumwona. Soma Luka 19:5-8. Kwa nini Zakayo anatoa nusu ya fedha zake kwa maskini?

1.  Zakayo hambainishi mtu mahsusi au huduma mahsusi. Kwa nini anatoa tu asilimia hamsini?

2.  Viongozi wa Kiyahudi walikuwa na maoni gani juu ya Zakayo? (Walimuita “mdhambi.” Soma Luka 19:2 inayotuambia kuwa alikuwa “mkubwa katika watoza ushuru.” Rumi ilitoa kandarasi ndogo (subcontracted) ya kukusanya kodi kwa watu binafsi kwa dhana ya kwamba mkusanya kodi atasalia na kiasi fulani cha makusanyo kama malipo yake. Ninahisi mtazamo wa wengi ulikuwa ni kwamba kwa ujumla Zakayo alikuwa anauibia umma. Hilo linaweza kuwa lilimhamasisha kusema kiholela kwamba atatoa nusu ya fedha kwa maskini.)

C.  Soma Mambo ya Walawi 25:35. Unadhani kauli ya “amekuwa maskini” inamaanisha nini? (Inaonekana kama ajali na sio mtindo wa maisha.)

1.  Maskini huyu alifanya nini hadi kustahili msaada? (Hakufanya chochote isipokuwa kwamba hii haikuwa hali ya kawaida ya mtu huyu.)

D.  Soma Ayubu 29:16-17. Ayubu aliwatendea maskini mambo gani matatu? (Aliwasaidia wale waliokuwa wahitaji. Zaidi ya hayo, aliwatafuta wale waliohitaji msaada. Mwisho, alipambana na wale waliowadhulumu maskini.)

E.  Rafiki, tunabarikiwa kwa kuwasaidia maskini. Lakini sehemu ya msaada huo ni kutopigia chapuo (kutohamasisha) uzembe na kuwahamasisha maskini jinsi ya kuishi maisha mazuri. Je, utajitoa kuwasaidia maskini, hususani wale ambao ni wanafamilia?

V.  Juma lijalo: Kupanga kwa Ajili ya Mafanikio.