Somo la 6: Kujiwekea Hazina Mbinguni
Somo la 6: Kujiwekea Hazina Mbinguni
(Mathayo 6, 13 & 19, Mwanzo 6 & 7)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, una hitaji la kuwa na mtu anayekufuatilia nyendo zako? Ninafahamu kwamba ninaye. Kila juma ninafundisha somo ninaloliandika. Hii ni hatua muhimu na ya thamani sana katika kuangalia na kuzichunguza fikra zangu. Malaki 3 (pamoja na vifungu vingine tulivyojifunza) inatuambia kuwa tukitoa mali zetu kwa ajili ya kazi ya Mungu, atatumwagia baraka kubwa. Ninafundisha kwamba baraka hizi ni za kifedha, miongoni mwa vitu vinginevyo. Wanakikosi wa darasa langu wanajibu kwa kusema kuwa baraka hizi zinahusu vitu vingine tofauti na fedha. Nani yuko sahihi? Wahusika wakuu katika Agano la Kale walikuwa matajiri na wahusika wakuu katika Agano Jipya hawakuwa matajiri. Mathayo 6:19-20 inayozungumzia juu ya fedha inaendana na mtazamo wangu. “Hazina ni sawa na fedha.” Aaa! Mimi ni mzee ambaye nimeweka akiba kwa ajili ya kustaafu kwangu. Lakini kama baraka zilizoelezewa katika Malaki 3 hazihusiani na fedha, je, tunapaswa kuhitimisha kwamba “hazina duniani” pia hazihusiani na fedha? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!
I. Asili ya Hazina
A. Soma Mathayo 6:19. Je, hii ni kauli inayoibua mjadala? (Hapana. Kanuni ya Pili ya Thermodynamics, kwa ufupi, inasema kwamba vitu vikiachwa vyenyewe vinaharibika sana. Sote tumeshuhudia hilo. Hazina zetu haziko salama hapa duniani.)
B. Soma Mathayo 6:20. Mbinguni ndipo mahala pakamilifu. Ninaamini kwamba Kanuni ya Pili ya Thermodynamics haifanyi kazi mbinguni. Swali halisi ni kwamba: “Tunawekaje mbinguni? “Tunajiwekeaje hazina mbinguni?” (Jibu kwa maswali hayo ndio mjadala mkuu unaofuata.)
C. Soma Mathayo 6:21. Je, hii inatusaidia kuelewa maana ya “hazina?”
1. Je, kitu chochote tunachokipenda zaidi ya Mungu kinaweza kufafanuliwa kama hazina? (Nina mashaka kama hilo ni kweli.)
2. Ili kusaidia katika uelewa wetu wa “hazina,” angalia tena Mathayo 6:19. Vitu gani vinaweza kupata kutu, kuliwa, na kuibwa? (Hii inaonekana kama Yesu anazungumzia vitu vinavyogusika. Lakini kama jambo hili litachukuliwa kiuhalisia, tutavifikishaje vitu hivi vinavyogusika mbinguni? Na kama tukiweza, je, tutavithamini huko mbinguni?)
D. Soma Mathayo 13:44. Hii inafafanua Ufalme wa Mbinguni kama hazina. Je, mambo yote hayo ni hazina?
1. Je, yanauzwa?
2. Hebu tuliangalie hili kwa mtazamo wa uhalisia. Kwa nini mtu anayeelezewa kwenye fumbo/kisa auze kila alichokuwa nacho ili kulinunua shamba? (Kwa sababu hazina iliyofichika katika shamba hilo ilikuwa na thamani zaidi ya fedha zake.)
a. Je, alitarajia kutengeneza faida? (Ndiyo!)
b. Je, matarajio hayo yanahusika na kwetu pia? Kwa mfano, kama tunaizungumzia fedha kama hazina, je, tunapaswa kupata fedha zaidi kwa kuupa kipaumbele Ufalme wa Mungu?
3. Kama mbingu ni hazina, je, inaleta mantiki kuhitimisha kwamba “kujiwekea hazina mbinguni” kwa kiasi kikubwa inamaanisha kufika mbinguni? Unapofika mbinguni tayari una hazina?
II. Kijana Mdogo Tajiri
A. Soma Mathayo 19:21. Je, tumefikia maelekezo sahihi kabisa juu ya kutengeneza hazina mbinguni? Tunaweka hazina mbinguni kwa kuuza vyote tulivyo navyo na kuwapa maskini?
B. Hebu tusome muktadha ili tuelewe vizuri zaidi fundisho la Yesu. Soma Mathayo 19:16. Unalifikiriaje swali hili? (Soma Waefeso 2:8-9. Hii inafundisha kuwa wokovu huja kwa njia ya imani na sio matendo. Kama tutakavyoona, kijana mdogo tajiri alikuwa anajivunia matendo yake, ambalo ndilo tatizo halisi lililobainishwa kwenye kifungu hiki.
C. Soma Mathayo 19:17. Hebu subiri kidogo! Unadhani kwamba Yesu aliamini kuwa tunaokolewa kwa kuzishika amri?
1. Je, Paulo (anayeandika katika kitabu cha Waefeso) na Yesu wanakinzana?
D. Soma Mathayo 19:18-21. Kijana mdogo tajiri anasema kuwa amezishika amri zote. Unadhani hilo ni kweli?
1. Soma Wagalatia 3:10-11. Hii inaashiria nini juu ya ukweli wa kauli ya kijana mdogo tajiri?
E. Soma Mathayo 19:22. Je, hii ndio amri ambayo kijana mdogo tajiri hakuishika? (Hakuwa tayari kuuza kila alichokuwa nacho.)
1. Kwani amri hii ni ipi ambayo Yesu anainukuu ikiwa imeandikwa katika Agano la Kale? (Sidhani kama ipo. Kimsingi Yesu anazielezea sheria. Lakini sheria ya Agano la Kale inayopatikana katika kitabu cha Walawi 19:18 ambayo Yesu anainukuu katika Mathayo 22:39-40 ni “mpende jirani yako kama nafsi yako.” Kamwe siwezi kumwambia jirani yangu kuuza kila alicho nacho na kunipatia. Tafakari tatizo halisi ikiwa kila mtu anatakiwa kuuza kila alicho nacho na kupeana na wengine. Mara ninapokupatia, unatakiwa kunirejeshea.)
2. Je, unadhani kwamba kijana mdogo tajiri angekuwa mkamilifu kama angeuza kila alichokimiliki na kuwapa maskini? (Soma tena Wagalatia 3:10-11. Hii inatuambia kwamba kwa kuwa kijana mdogo tajiri hakuweza kutii kikamilifu kwa kuuza kila alicho nacho, alikuwa chini ya laana.)
a. Kijana mdogo tajiri aliishiaje kuwa chini ya laana? (Kwa kuwa mtu “aliyetegemea matendo ya sheria.”)
F. Soma Mathayo 19:23-24. Hatutaki kupoteza mwelekeo wa suala hili. Je, Yesu anasema (Mathayo 19:21) kwamba njia ya kuweka hazina mbinguni ni kwa kuuza kila tulicho nacho na kuwapa maskini? (Sidhani. Badala ya kusababisha ukinzani na kauli za Kibiblia za Paulo, Yesu anafafanua kile ambacho Paulo anakiandika – hakuna anayeweza kuishika sheria kikamilifu – na ukijaribu kufanya hivyo utashindwa na kuishia kuwa chini ya laana.)
1. Unaelezeaje kile anachokisema Yesu kuhusu ugumu wa mtu tajiri kuingia mbinguni? (Mtu Tajiri anashawishika kuzitumaini fedha zake badala ya kumtumaini Mungu.)
2. Je, huo sio ufunguo wa dhahiri sana wa kuweka hazina mbinguni – kumtumaini Mungu? (Litafakari hili. Kama Yesu angekuwa anazungumza kiuhalisia, kwamba lazima matajiri wauze vyote walivyo navyo ili wawe wakamilifu kuingia mbinguni, basi hakuna mtu tajiri hata mmoja atakayeingia mbinguni. Mbingu haitaingiwa na matajiri wenye “ugumu,” hawataingia kabisa.)
III. Nuhu
A. Soma Mwanzo 6:13-15, Mwanzo 6:18, na Mwanzo 7:6-7. Chukulia kwamba kamwe hujawahi kukisikia kisa hiki. Utakuwa na mwitikio gani kwenye amri ya Mungu ya kujenga hii boti kubwa?
B. Soma 2 Petro 3:3-6. Hii inaashiria kuwa dunia ya kipagani ilifanya nini wakati Nuhu alipokuwa akijenga Safina? (Dhana ya maji kuifunika dunia ilikuwa sio ya kuaminika sana kiasi kwamba inawezekana Nuhu alikabiliana na wadhihaki.)
C. Chukulia kimantiki, kutokana na misingi ya vifungu hivi, kwamba Nuhu alishangazwa na amri ya Mungu kutengeneza boti kubwa na watu waliomzunguka Nuhu walikuwa wakimdhihaki kwa namna ambavyo wapagani wanadhihaki juu ya dhana ya mwisho wa dunia. Nuhu anatakiwa kufanya nini kama alivyoelekeza Mungu? (Nuhu atahitaji tumaini/imani kamili kwa Mungu.)
1. Je, Nuhu alipokea hazina kutokana na imani yake? (Soma Mwanzo 7:23. Nuhu na familia yake waliirithi dunia yote.)
2. Tumejadili dhana ya kwamba mbingu ndio hazina halisi inayojadiliwa, na tumaini ndio ufunguo wa kuipata hazina hiyo. Je, unadhani kisa cha Nuhu kinafafanua dhana ya “hazina mbinguni?” (Nadhani kinafafanua. Nuhu alimtumaini Mungu na aliirithi nchi. Hii inaendana na tumaini letu kuhusu mbingu.)
IV. Hubiri Mlimani
A. Mathayo 6:20, kifungu kinachohusu kujiwekea hazina mbinguni, ni sehemu ya Hubiri Mlimani. Hebu tuchunguze alichokisema Yesu mara baada ya hapo. Soma Mathayo 6:24-25. Yesu anazungumzia nini kuhusu fedha? Anazungumzia nini kuhusu tumaini? (Kama tuko sahihi kwamba kujiwekea hazina mbinguni kunahusiana na tumaini, sasa Yesu anarudia ujumbe wa kwamba tukizitumaini fedha “tutadharau” kumtumaini Mungu. Kushindwa kumtumaini Mungu hutufanya kuwa na wasiwasi.)
B. Soma Mithali 10:3-5. Hii inatufundisha nini kuhusu bidii ya kazi na mipango? (Kuwa na juhudi na kuwa na mipango hukutajirisha na kuwa mvivu hukufanya kuwa maskini. Chagua kuwa na juhudi na busara.)
C. Rafiki, hatutakiwi kutumaini matokeo ya jitihada zetu. Tukifanya hivyo hatutamtumaini Mungu. Kumtumaini Mungu, na sio fedha, ndio ufunguo wa kwenda mbinguni. Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie umtumaini Mungu?
V. Juma lijalo: Kwa Mmojawapo wa Hao Walio Wadogo.