Somo la 2: Maagano ya Mungu na Sisi

Mathayo 6, Malaki 3, 2 Wakorintho 9
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
2

Somo la 2: Maagano ya Mungu na Sisi

(Mathayo 6, Malaki 3, 2 Wakorintho 9)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

`Utangulizi: Kitabu cha Warumi 5 kinarejelea mara kwa mara juu ya kuhesabiwa kwetu haki mbele ya Mungu kama neema. Kama tulikanganyikiwa juu ya maana ya “neema ya bure,” kwa kujirudiarudia inarejelewa kama “wingi wa neema.” Angalia, kwa mfano, Warumi 5:17. Licha ya hayo, baadhi ya watu wanaendelea kuuliza “Kuipokea neema kunatutaka tufanye nini?” Haitakuwa neema “nyingi” kama ingetutaka tutende jambo fulani. Hata hivyo, kuna mambo mawili yanayokaribiana sana. Swali la la uhalisia ni kama, je, tunaitaka neema? Watu wengi hawatakubali neema ya bure ya kuwa mshirika wa ukumbi wa michezo ya mazoezi ya viungo (gym) kwa kuwa wanaelewa lengo la gym. Watu wengi hawaupendi uzima wa milele kwenye Ufalme unaotawaliwa na Mungu. Hivyo, swali lenye mantiki ni hili: “Je, kweli unataka neema nyingi ya uzima wa milele katika nchi itakayofanywa upya?” Kuuliza kama kweli unatamani neema haibadili ukweli kwamba hupatikana bure. Swali la pili linalohusiana na hilo ni somo letu la juma hili. Kwa nini Mungu anatuamrisha tutende (au tusifanye) mambo fulani? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

I.  Kutandika Kitanda Sio Kazi Yako ya Kwanza

A.  Soma Mathayo 6:33. Tunatakiwa kutafuta nini kwanza kila siku? (“Ufalme wa Mungu na haki yake.”)

1.  Unadhani hii inamaanisha nini? (Kwanza fanya mambo ambayo yanautangaza ufalme wa Mungu. Kwa kuwa haki ni neema ya bure, maelekezo ya Yesu kwamba tuitafute inamaanisha kuenenda kila siku katika maisha ya haki.)

2.  Ushauri kwa vijana kwamba jambo la kwanza wanalopaswa kulifanya kila siku ni kutandika vitanda vyao ni ushauri wa uhalisia. Unalinganishaje ushauri huu na ushauri wa Yesu? (Omba kabla hujatandika kitanda chako!)

B.  Angalia msitari wa mwisho wa Mathayo 6:33. “Hayo yote” yaliyoahidiwa ni mambo gani? (Kwa jibu hilo tunatakiwa kuchimbua muktadha wa awali. Hebu tufanye hivyo katika sehemu inayofuata.)

II.  Maisha Toshelevu

A.  Soma Mathayo 6:25. Wasomaji wangapi wana wasiwasi juu ya mamho haya? Si utakuwa masikini sana ili kuwa na wasiwasi juu ya masuala ya msingi ya kula, kunywa, na nini cha kuvaa? (Yumkini wasomaji wengi hawana wasiwasi sana juu ya mambo haya.)

B.  Soma Mathayo 6:26 na Mathayo 6:28-30. Yesu anatoa jibu gani kwenye suala la wasiwasi? (Upendo wa Mungu kwako. Mungu anawapenda ndege na maua, na anakupenda. Viumbe hao ni wazuri nawe pia utakuwa barabara.)

C.  Soma Mathayo 6:27. Ninahisi hili linaeleweka zaidi kwa wasomaji wengi. Je, una wasiwasi juu ya urefu wa maisha yako? 

1.  Tunapaswa kuwa na wasiwasi juu ya urefu wa maisha yetu kwa kufanya mazoezi, kula kwa usahihi, kuvaa mikanda, na kutovuta sigara. Yesu anazungumzia nini? (Neno la msingi ni “wasiwasi.” Dukuduku ni wasiwasi usio na mashiko. Hairejelei kuchukua tahadhari stahiki.)

D.  Soma Mathayo 6:32-33. Elezea kile wanachokifanya Mataifa na wafuasi wa Yesu hawakifanyi? (Huu ni mgawanyiko mkubwa. Wapagani wanahaha kutafuta chakula, mavazi, na maisha. Mungu anawapa vitu hivi moja kwa moja wale wanaoutafuta kwanza ufalme wake.)

1.  Utaona kwamba somo hili linarejelea “maagano” ya mikataba. Je, Yesu anatupatia mkataba? Mtafute kwanza naye atakuhudumia?

E.  Soma Mathayo 6:34. Mara ngapi umekuwa na wasiwasi kwamba jambo baya litakutokea katika siku za mbele na kamwe halikutokea?

III.  Maisha ya Usitawi

A.  Soma Malaki 3:10. Unadhani “zaka kamili” ni kitu gani? (Zaka ni moja ya kumi ya kitu fulani. Pendekezo ni kwamba watu walikuwa na mwelekeo wa kudanganya kwenye hili suala la 10%.)

1.  Matokeo ya kutoa “zaka kamili” ni yepi? (Unabarikiwa hadi kufikia kiasi cha kutohitaji chochote.)

2.  Je, huu ni mkataba? (Angalao ni mkataba. Mungu anasema “tumjaribu,” ambapo ni ukaribisho wa kupokea ofa yake.)

B.  Soma Malaki 3:11. Kama ungekuwa mkulima, ungekuwa na udhibiti gani juu ya “mharibifu?” Ungekuwa na udhibiti gani juu ya endapo mazao yako yatazaa matunda? (Haya yanaonekana kuwa mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yako nje ya uwezo wa mkulima. Kutokana na hili ninaelewa Mungu akisema kwamba atayadhibiti mambo hayo ambayo hatuna udhibiti nayo.)

C.  Soma Malaki 3:12. Watu wengine watayachukuliaje maisha yako? (Umebarikiwa. Kuyaishi maisha yako ni jambo la furaha.)

1.  Je, kurejelea mtu binafsi ni tatizo kwa kuwa suala hili linarejelea taifa?

D.  Soma Malaki 3:13-14. Je, una mashaka juu ya kile tulichokisoma hivi punde katika kitabu cha Malaki? (Vifungu hivi ni onyo dhidi ya kuitia changamoto ahadi ya Mungu linapokuja suala la kutoa zaka.)

E.  Soma Malaki 3:15. Madai ya wenye mashaka ni yepi? (Wenye viburi na watenda maovu wanasitawi na Mungu hafanyi chochote juu ya hilo.)

1.  Unadhani Mungu anawashutumu wenye mashaka, au anatarajia ukosoaji wa ofa yake ya zaka? Au, vyote viwili?

F.  Soma Malaki 3:16-17. Je, kitabu cha Malaki kimehamia kwenye mada nyingine? Au, mada hii inahusiana na mjadala wa zaka? (Hii inahusiana. Mungu anatoa ahadi ya baraka ambazo zinaweza zisitimie kikamilifu katika kipindi cha uhai wetu.)

G.  Soma Malaki 3:18. Je, ahadi ya zaka inatimia mbinguni pekee? (Hapana! Kifungu kinasema “kwa mara nyingine mtaona tofauti kati ya [watu wema na wabaya].” Utoaji zaka thawabu yake huonekana hapa hapa tena sasa hivi.)

H.  Hebu tujiulize maswali magumu zaidi. Tutaliangalia hili kwa kina katika somo linalofuata. Hekalu (na ghala lake) havipo tena. Hatuna tena ule mfumo wa kikabila ambapo Walawi na makuhani wanajikimu kwa zaka. Na Agano Jipya haliwaambii Mataifa chochote juu ya utoaji zaka. Kwa kuzingatia hili, je, bado utoaji zaka unahitajika? 

I.  Soma 2 Wakorintho 9:6-9. Hapa unaona kanuni gani kuhusu kuchangia kwenye kazi ya Mungu? (Hatuoni tarakimu ya lazima, 10%, badala yake kifungu kinasema “toa” kama ulivyodhamiria moyoni mwako.)

1.  Tulipokuwa tunajadili juu ya zaka, sehemu ya changamoto ya Mungu iliyokugusa zaidi ni ipi? (Baraka.)

2.  Je, hilo limebadilika? (Bado hilo ni jambo kuu – ukipanda haba, utavuna haba. Ukipanda kwa ukarimu, utavuna kwa ukarimu. Ukimtolea Mungu naye anaahidi kukubariki!)

J.  Soma 2 Wakorintho 9:10-11. Hebu rudi nyuma na utafakari jinsi ambavyo ungeenenda kwenye ahadi za 2 Wakorintho 9:6-7 kwa kuzingatia kauli za Malaki 3. Utatoa kiasi gani? (2 Wakorintho 9:7 inasema kuwa unafanya uamuzi, lakini zingatia kwamba 10% ni alama ya kihistoria ya Mungu. Jambo la muhimu zaidi, mada isiyobadilika ni kwamba kumtolea Mungu hakukugharimu chochote. Unachokitoa kinarejeshwa maishani mwako kama baraka. 2 Wakorintho 9:11 inaahidi kuwa “mtatajirishwa katika vitu vyote” – jambo litakalokufanya muwe wakarimu zaidi.)

K.  Soma 2 Wakorintho 9:12. Lengo la utoaji ni lipi? (Mahitaji ya watakatifu na kuonesha shukurani kwa Mungu.)

L.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 7:13-14. Tunapaswa kuzingatia jambo gani la ziada kuhusu kuishi maisha ya baraka? (Suala sio kutoa fedha kwa ajili ya kazi ya Mungu, tunatakiwa kuwa watiifu wa mapenzi yake.)

1.  Hebu tupitie upya sehemu ya utangulizi ya somo hili. Wokovu ni zawadi ya bure. Kisicho cha bure, kitu gani kinayategemea matendo yetu? (Tumeona kwamba Mungu anaingia “mkataba” nasi kwamba tukiutafuta kwanza ufalme wake, tukiwa wakarimu kwa fedha zetu katika kuitegemeza kazi yake, tukizitii amri zake, atatupatia maisha ya baraka na yaliyo tele.)

2.  Je, hii ni ahadi inayotolewa kwa kila aaminiye? (Waebrania 11 na kisa cha Ayubu vinatuonesha kuwa hii ni kanuni ya jumla ya maisha, lakini muda wa Mungu unaweza na utabadilika hadi uovu wote utakapoangamizwa.)

M.  Rafiki, mimi ni uthibitisho wa kwamba matokeo ya kuwa mkarimu kwa Mungu ni kubarikiwa hapa duniani. Maishani mwangu mwote nimefanya kazi kwenye shirika lifanyalo kazi si kwa kupata faida (non-profit) kutangaza kanuni ya Ufalme wa Mungu. Mimi na mke wangu tulipooana, na huku tukiwa masikini sana, tulitoa zaka mara mbili. Mara zote nimekuwa nikichukulia kiwango cha 10% kuwa kiwango cha chini cha kumtolea Mungu. Mimi na mke wangu sasa tumezeeka na tunaishi kwa “kipato kamili,” lakini mke wangu ana moyo wa pekee wa kutoa fedha ili kusaidia kuutangaza Ufalme wa Mungu na “watakatifu.” Roho Mtakatifu anauongoza moyo wake kwenye utoaji, na mara zote tunashangazwa na baraka endelevu za Mungu. Kwa nini usifanye uamuzi sasa hivi kuwa mkarimu kwa Mungu?

IV.  Juma lijalo: Mkataba wa Zaka.