Somo la 11: Udanganyifu wa Wakati wa Mwisho

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Waefeso 6, 2 Wakorintho 11, Luka 9, 1 Samweli 28
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
4
Lesson Number: 
11

Somo la 11: Udanganyifu wa Wakati wa Mwisho

(Waefeso 6, 2 Wakorintho 11, Luka 9, 1 Samweli 28)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Ninapotunga mtihani wa mwisho kwa wanafunzi wangu wa shule ya sheria huwa ninaongezea kwenye swali kauli za kweli zisizo na umuhimu wa kisheria. Hii huwasaidia wanafunzi kujiandaa na maswali ya wateja. Mteja anakuja na kisa chake huku akibainisha kwa nini anadhani kuwa ana madai ya kisheria. Ni kazi ya mwanasheria kuchekecha na kufanya uchunguzi wa kina wa kisa hicho na kubainisha kweli zipi zinaleta utofauti na zipi zisizo na mashiko. Hadi kufikia hapa mfululizo wa masomo yetu kwa kiasi kikubwa umeshughulika na mauti, kufariki, na mbingu. Kuna “kweli” nyingi zinazozagaa kwenye vitabu, sinema, televisheni, na ushuhuda ambao unatakiwa kutathminiwa kwa umakini. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza juu ya kuzifanyia tathmini “kweli” hizi!

I.  Kuwa na Uzingativu Sahihi

A.  Soma Waefeso 6:10-12. Adui wetu wa kiroho ni nani? (Ni Shetani na malaika wake walioanguka.)

1.  Litafakari hilo. Unapaswa kuzingatia nini maishani mwako? (Hatutakiwi kujikita katika kugombana na watu, tunapaswa kujikita juu ya “hila za Shetani.” Tunatakiwa kuangalia zaidi ya mambo ya mtu na kutafakari suala la kiroho.)

B.  Soma 2 Wakorintho 11:10-12. Hapa jambo gani linaonekana kuwa tatizo ambalo Paulo analijadili? (Ana washindani ambao pia wanadai kufanya kazi nzuri.)

C.  Soma 2 Wakorintho 11:13-15. Tulipojadili suala la kutafakari masuala ya kiroho, na sio mambo ya mwanadamu, je, kifungu hiki kinaongezea jambo la muhimu kwenye mjadala wetu? (Naam! Hii inatuambia kuwa kimsingi “mwanadamu” anaweza kuwa malaika mpotovu anayeonekana kama mwanadamu. Pia inatuambia kuwa wanadamu wanaweza kuwa mawakala hai wa Shetani. Hii inamaanisha kuwaa tunatakiwa kutafakari changamoto za kibinadamu na kiroho, lakini suala la jumla ni ujumbe wa kiroho.)

1.  Inamaanisha nini katika kifungu cha 15 pale kinaposema, “mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao?” Kwa namna yoyote ile, hatimaye watahukumiwa na Mungu.)

D.  Soma Luka 9:46-48. Je, ni asili ya mwanadamu kati ya wafuasi wa Mungu kushindana miongoni mwao? (Hawa ni viongozi wajao wa kanisa la awali na ni washindani.)

1.  Je, Yesu anasema kuwa ushindani huu haufai? (Hapana. Anamrejelea “yeye aliye mkubwa.” Lakini, Yesu anasema huduma ndio njia ya kuufikia ukubwa.)

a.  Rejea ya mtoto mdogo inazungumzia nini juu ya asili ya kuhudumia wengine? (Bila shaka visa vya siku hiyo vilihusiana na mashujaa waliotenda mambo makuu. Yesu anafundisha kwamba huduma katika mambo madogo madogo ni ya muhimu kwake.)

E.  Soma Luka 9:49-50. Hadi kufikia hapa, tumejifunza kuwa tunapaswa kujikita kwenye mambo ya kiroho, lakini pia wanadamu wanaweza kuwa mawakala wa Shetani au malaika halisi walioanguka. Pia tumejifunza juu ya kuwa makini kuhusu ushindani miongoni mwa viongozi. Mjadala huu juu ya washindani “nje” ya kanisa unatufundisha nini kuhusu kuzitenganisha kweli? (Kwa kuwa tu kiongozi wa kiroho yuko nje ya kundi letu (nje ya madhehebu yetu) sio ishara ya kwamba anatenda uovu. Katika kutenganisha ukweli na uongo tunatakiwa kuangalia aina ya kazi. Sio lazima iwe kazi ya hadhi ya juu, na sio lazima iendane kikamilifu na kazi yetu. Kazi pekee inayopingana nasi ndio tatizo. Kipingamizi chetu kinaweza kuakisi ushindani tu na sio uovu wa kiroho.)

II.  Kutenda kwa Usahihi

A.  Soma 1 Samweli 28:3. Samweli alikuwa nani? (Alikuwa nabii wa Mungu ambaye alimshauri Mfalme Sauli mara kwa mara. Angalia 1 Samweli 15:1.)

1.   Wenye pepo wa utambuzi na wachawi ni watu gani? (Soma Kumbukumbu la Torati 18:11, Mambo ya Walawi 20:27, na Mambo ya Walawi 20:6. Hawa ni watu wanaodaiwa kuwasiliana na wafu. Hili ni eneo la dhambi mbaya kabisa.)

B.  Soma 1 Samweli 28:5-6. Sauli anakabiliana na tatizo gani? (Jeshi pinzani linalomtisha, na Mungu kukataa kumpa mwongozo.)

C.  Soma 1 Samweli 28:7. Unalinganishaje kampeni ya Sauli dhidi ya wenye pepo wa utambuzi na wachawi na hamu yake kubwa ya kuzungumza nao? (Sauli amekata tamaa.)

D.  Soma 1 Samweli 28:8-9. Je, mwanamke huyu mwenye pepo wa utambuzi ana wasiwasi juu ya hukumu ya kifo? Unadhani anashuku kama huyu ni Sauli au mmojawapo wa mawakala wake?

E.  Soma 1 Samweli 28:10-12. Kwa nini uwepo wa Samweli unamfanya mwenye pepo wa utambuzi adhani kuwa huyu ni Sauli? (Kwanza, ilijulikana kwamba Samweli alikuwa mshauri wa mfalme. Pili, “pepo” huyu hakuwa kitu walichokiwazia, kilikuwa kitu kilichoonekana kuwasiliana na mwenye pepo wa utambuzi kuhusu ukweli juu ya Sauli.)

F.  Soma 1 Samweli 28:15. Unalichukuliaje jibu la Sauli kwenye swali la Samweli? (Sauli anakiri kwamba Mungu hatazungumza naye.)

1.  Sauli anadhani kuwa anazungumza na nani? Samweli alipomshauri, Samweli alikuwa anafikisha ujumbe kutoka kwa Mungu! (Hili halina mantiki yoyote isipokuwa tu kama Sauli anadhani kwamba anaweza kumshinda Mungu kiakili kwa kuzungumza na Samweli kwa njia hii.)

G.  Soma 1 Samweli 28:16-18. Je, huu ndio ukweli – kwamba Mungu amemwacha Sauli na kumpa ufalme wake mtu mwingine? (Ndiyo. Soma 1 Samweli 15:26-28.)

1.  Je, hizi ni taarifa ambazo Sauli (pamoja na wengineo wengi) tayari walizifahamu? (Ndiyo.)

2.  Kwa hiyo, Sauli anazungumza na nani? (Hazungumzi na Mungu. Mungu hazungumzi na Sauli kwa namna yoyote ile. Angalia 1 Samweli 28:15. Hivyo huyu hawezi kuwa Samweli.)

H.  Soma 1 Samweli 28:13-14. Hapo kabla tuliruka vifungu hivi. “mungu” gani anatoka katika nchi? (Huyu ni Shetani au malaika mpotovu tukichukulia sura ya Samweli. Je, Samweli aliyekufa anaweza kuvaa vazi? Je, anaweza kumkana Mungu na kuzungumza na Sauli?

I.  Soma 1 Samweli 28:19-20. Je, Shetani anaweza kutabiri mambo yajayo? Ikiwa sivyo, je, hii inathibitisha Samweli anazungumza maneno ya Mungu? (Sauli na chochote kile kilichotoka katika nchi walijua kwamba Mungu hataongea na Sauli. Pia wote wawili walijua kwamba Mungu alimnyang’anya Sauli ufalme na kumpatia Daudi. Hiyo ilimaanisha kwamba Sauli na wanaye wanapaswa kufa – na hicho ndicho kiinachotaarifiwa baadaye katika 1 Samweli 31:6. Na kwa kuongezea tunaona madhara ya kutisha ya kisaikolojia yanayosababishwa na maneno haya. Sio lazima uwe nabii wa Mungu ili kujua jinsi mambo haya ambavyo yangetokea.)

J.  Soma tena 2 Wakorintho 11:14-15. Kifungu hiki kinaoanaje na kisa tulichokijadili hivi punde? (Hii inaonesha kwamba Shetani au mmojawapo wa malaika wake walioanguka pamoja naye alijigeuza na kuwa kama Samweli.)

1.  Hebu tutumie mahitimisho haya kwenye kweli zinazodaiwa leo. Tunapaswa kuhitimisha nini kuhusu watu wanaotuambia kuwa mababu wao waliofariki huwatokea? Au kutokea kama ndege au vipepeo ili kutoa ujumbe wa kutia moyo? (Tunaweza kuhitimisha kwamba wanachokiona ni kitu halisi – lakini sio ndugu zao waliofariki. Badala yake, hizi ni pepo. Kuhitimisha kwamba ndugu yako ni mdudu au ndege ni kufanya fikra yako iwe na wazimu.)

2.  Vipi kuhusu watu wenye “uzoefu wa matukio yanayokikaribia kabisa kifo” wanaoeleza habari za kuona nuru, kusafiri kwenda mbinguni, na kuzungumza na ndugu aliyefariki au Yesu? (Kama tulivyoona kwa Sauli, inawezekana kabisa watu hawa wameona kitu fulani, lakini kitu hicho hakikuwa ndugu yao aliyefariki. Utaona pia kwamba mara nyingi watu hawa huwa wamepungukiwa hewa ya oksijeni, na hivyo mawazo yao yanaweza yasiwe yanafanya kazi vizuri.)

3.  Tulikubaliana mwanzoni mwa somo hili kwamba suala la muhimu kabisa la kulizingatia ni lipi? (Suala la kiroho.)

a.  Sauli alipozungumza na mungu aliyetoka katika nchi, je, mungu huyo alimwambia Sauli mambo mengi yaliyokuwa ya kweli? (Karibia yote yalikuwa ya kweli.)

b.  Shetani alikuwa na lengo gani katika mazungumzo haya ikiwa alimwambia Sauli ukweli? (Lengo lilikuwa ni kumdhuru Sauli. Alitaka Sauli ateseke. Alitaka kumkatisha tamaa Sauli. Alitaka kuwadhuru watu wa Mungu. Yote hayo yalitokea.)

K.  Hebu turejee pale tulipoanzia. Kweli zipi ni za muhimu na za maana kwa wale wanaodai kuwa wamezungumza na wale waliofariki? (Huenda wanasema ukweli, lakini hawaelewi kwamba hawazungumzi na wafu, bali wanazungumza na pepo. Pepo wanaotaka kuwadhuru.)

L.  Rafiki, dhana ya kwamba wafu wapo wanatuzunguka na wanaweza kutusaidia ni uongo. Huyu si mwingine bali ni Shetani na watumishi wake wakitenda kazi kuwadhuru wafuasi wa Mungu. Baadhi ya mambo hayo ni halisi (jambo halisi linaonekana), baadhi ya mambo hayo hunena ukweli. Lakini kuliangalia jambo hilo kwa muktadha wa kiroho, lengo la Shetani ni kukudhuru wewe na familia yako. Je, utadhamiria leo kukataa na kuepuka taarifa hizi na mambo haya ya umizimu wa kisasa?

III.  Juma lijalo: Falsafa ya Maisha ya Kibiblia.