Somo la 6: Alikufa kwa Ajili Yetu
Somo la 6: Alikufa kwa Ajili Yetu
(Ufunuo 13, Warumi 1, Yohana 3 & 19)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mwaka 2004 nilihudhuria Kongamano la Kitaifa la Kidini (National Religious Broadcasters Convention) na kutazama nakala ya awali ya “The Passion of the Christ” iliyoandaliwa na Gibson. Niliporejea hotelini kwangu nilipiga magoti kwa masikitiko kwa ajili ya dhambi zangu na kumshukuru Yesu kwa kile alichonitendea pale msalabani. Ingawa ninayo nakala ya sinema ile, zijawahi kuitazama tena kwa sababu inahuzunisha sana na kuumiza hisia. Litafakari jambo hilo. Alichokifanya Shetani kwa Yesu, na kile ambacho Yesu alikikubali na kukipokea kwa hiari kinaogofya sana kiasi kwamba hata sitaki kuitazama tena sinema hiyo. Somo letu la Biblia juma hili halizungumzii juu ya kafara ya kutisha ya Yesu, bali kile ambacho mpango huu wa wokovu wetu unakizungumzia kuhusu Bwana wetu na jinsi tunavyopaswa kuuitikia. Hebu tuzame kwenye somo letu!
I. Msingi
A. Soma Ufunuo 13:7-8 na Matendo 2:23. Vifungu hivi vinasema kuwa kifo cha Yesu msalabani kilipangwa mbinguni “tangu kuwekwa misingi ya dunia.” Mpango huu ulikuwa unazungumzia tatizo gani? (Kwamba wanadamu wanaweza kutenda dhambi.)
1. Jiweke kwenye nafasi ya Mungu. Mipango gani mbadala ingeweza kuzingatiwa?
2. Tuchukulie kwamba tunashughulikia tatizo la motokaa yako. Kwa nini utatue tatizo kwa njia inayotumia gharama kubwa zaidi na isiyofurahisha? (Lazima Mungu alifanya uamuzi kwa kuzingatia kuwa hapakuwepo na njia nyingine ya kutatua tatizo.)
a. Kweli? Njia rahisi ya kuepuka tatizo hili ingekuwa ni kuachana na kuwaumba wanadamu. Kuna tatizo gani kwenye hilo suluhisho rahisi? (Jibu pekee ni kwamba Mungu alitupenda sana kiasi kwamba hakuwa tayari kulikubali suluhisho hilo.)
b. Suluhisho jingine ni kuweka ukomo wa uhuru wa uchaguzi. Kuna tatizo gani kwenye suluhisho hilo? (Kiini cha upendo ni uhuru wa uchaguzi.)
B. Angalia tena Ufunuo 13:8. Tafsiri ya ESV inakielezea kifungu hiki kwa utofauti kidogo. Kinasema kuwa majina yaliandikwa katika Kitabu cha Uzima kabla ya kuwekwa msingi wa dunia. Je, hii inaunga mkono dhana ya kwamba Yesu alikubali kufa kwa sababu Mungu anatupenda? (Kwa kuwa jina lako liliandikwa kwenye Kitabu cha Uzima katika kipindi ambacho Mungu Baba alishafanya uamuzi juu ya mpango wa wokovu, mpango huo uliandaliwa mahsusi kwa ajili yako!)
1. Tunapaswa kulielewaje hili: kwamba Mungu aliandika jina la kila mtu katika Kitabu cha Uzima na kama jina lako likiondolewa, ni kwa sababu ya uamuzi wetu wa kusababisha jina hilo kuondolewa? Au, kwamba mara zote Mungu anajua nani atakayempokea na kumkubali?
a. Ukichagua chaguo la pili, je, hiyo inamaanisha kuwa mpango wa wokovu ulifahamika kabla, na kwamba kimsingi ulipangwa mapema?
2. Je, unadhani kwamba Mungu alishangazwa na jinsi Shetani na malaika walioanguka walivyogeuka na kuwa na nia mbaya pale msalabani?
C. Soma 1 Petro 1:18-19 na Yohana 1:29. Kwa nini Mungu aliweka mpango kwamba kabla ya Yesu kuja duniani watu wake watatoa kafara ya kondoo kwa ajili ya dhambi zao? (Mfumo wa kafara uliashiria kile ambacho Yesu atakifanya.)
1. Hebu tuchimbue maswali kadhaa kuhusu jambo hili. Je, watu wa Mungu walitoa kafara ya kondoo kwa namna yenye maumivu makubwa sana? (Hakuna uthibitisho wa hilo. Kinyume chake ndio ukweli.)
a. Kwa nini basi Yesu alikufa kifo chenye maumivu makali kiasi hicho? (Mpango wa Mungu haukuwa kumuumiza Yesu kwa maumivu makuu, huo ulikuwa mpango wa Shetani.)
b. Kafara ya kondoo iliwaathirije wadhambi? (Fikiria kwamba ulipaswa kumuua mnyama wa kufugwa kila mara ulipotenda dhambi. Nadhani hilo lingekuwa na athari kubwa kwetu.)
II. Mwitikio Wetu kwa Mwana-Kondoo
A. Soma Warumi 1:18 na Warumi 1:26-28. Ninawapenda wanangu. Katika mojawapo ya mazungumzo ya hivi karibuni nimepewa changamoto kwa madai ya kwamba kanisa halidhihirishi upendo wa Mungu, aina ya upendo walionao wazazi, kwa watoto wanaosema kuwa ni mashoga. Kafara ya kondoo inatufundisha nini juu ya namna sahihi ya kutatua tatizo hili?
1. Utaona kwamba Warumi 1:18 inaonya dhidi ya kuupinga ukweli na Warumi 1:28 inaonya dhidi ya kumkataa Mungu. Hii inaongezea nini kwenye mjadala?
B. Soma Warumi 1:29-32. Hakuna mtu hata mmoja anayejadiliana nami juu ya mwitiko wa kanisa kwenye dhambi hizi. Kafara ya kondoo inazungumzia nini juu ya njia bora ya kushughulikia matatizo haya? (Upendo kwa watoto wetu, na kuzipenda dhambi zetu, hutuzuia kuwa na mtazamo wa kweli ambao unabainishwa na kumchinja mnyama.)
C. Linganisha 1 Wakorintho 5:9-11 na Mathayo 9:10-12. Kafara ya kondoo inatumikaje hapa? (Ni muhimu sana kufanya hili kuwa na utofauti.)
D. Soma Mathayo 16:21-23. Yesu anaelezea utume wake kama kondoo. Petro anamkemea Yesu. Kwa nini? (Yesu anafafanua kwamba mawazo ya Petro yamewekwa juu ya “mambo ya wanadamu” badala ya “kuyawaza mambo ya Mungu.”)
1. Unadhani Yesu anamaanisha nini? Ni nini kiini cha kosa la Petro? (Petro haelewi kafara ya kondoo. Sio tu kwamba tukio hili la kutisha lina athari ya kututoa dhambini, bali pia linapaswa kutupatia mtazamo wa kujikana nafsi.)
E. Soma 1 Wakorintho 2:6-8. Hapa tunaona kwamba “watawala wa dunia hii,” kama ilivyo kwa Petro, hawakuielewa kafara ya kondoo. Ni hekima gani hii ambayo ni ya “siri na imefichwa” na imeanzishwa na Mungu “tangu milele?” (Hii ni tofauti kati ya kupokea na kutoa kwa akili. Hatimaye Yesu anapata kila kitu – na hilo linaendana na hekima hii ya siri. Utafakari mfano wa familia inayofanya kazi kwa juhudi ili kutengeneza aina mpya ya kompyuta. Wanatajirika kutokana na kujitoa kwao kwingi, lakini wanayaboresha maisha ya wale wote wanaonufaika kutokana na matumizi ya kompyuta inayopatikana kiurahisi.)
III. Ushindi Thabiti wa Mwana-Kondoo
A. Soma Yohana 19:30. Kitu gani kilikwisha? Je, Yesu alikuwa anayazungumzia maisha yake? (Kama Yesu alikuwa anayazungumzia maisha yake angesema “Nimekwisha.” Kilichokwisha ni Msingi uliokubalika kabla wanadamu hawajaumbwa.)
1. Yesu ametimiza nini hadi kufikia hapa? (Amerejesha fursa yetu ya kurejesha uhusiano wetu na Yeye kama ilivyokuwa kipindi cha Edeni. Ameonesha kwamba Shetani hayuko sahihi, na kuyachukua mamlaka yake juu ya dunia. Ameithibitisha sheria.)
2. Hebu turejee kwenye mjadala tuliokuwa nao kwa kuzingatia somo la tatu katika mfululizo wa masomo haya. Yesu alisalimu roho gani katika Yohana 19:30? (Isingeweza kuwa Roho Mtakatifu. Badala yake, Yesu alirejesha kwa Mungu (katika asili yake ya uanadamu) utambulisho ule wa pekee ambao Mungu alimpatia Yesu tumboni mwa Mariamu.)
3. Kwa nini kifungu kinasema kuwa Yesu “akaisalimu roho yake?” Hii inaonekana kama ni jambo la hiari, lakini kwa wanadamu sio jambo la hiari. (Hii inaakisi kwamba Yesu pia alikuwa Mungu kamili. Alipata ushindi dhidi ya dhambi. Aliyabakiza mamlaka juu ya uhai.)
B. Soma Yohana 19:41-42. Kwa nini Yesu aliwekwa kaburini? Tumeona kwamba yote haya yalitokana na mpango mkuu. Tafakari jinsi ambavyo ingekuwa na utukufu, jinsi ambavyo ingekuwa na ushawishi, endapo mara baada ya kufa angefufuka na kuruka kutoka msalabani mbele ya macho ya wadhihaki na wenye kukejeli wote. Kwa nini hilo halikufanyika? (Kama ningekuwa Mungu Baba ningetaka kumkumbatia Yesu mara moja. Ningemliwaza kwa sababu alipitia mateso makali, na ningemkumbatia kwa sababu alishinda Medali Kuu ya ulimwengu.)
C. Soma Mwanzo 2:1-3. Unadhani ufafanuzi wa Yesu kupumzika kaburini unahusiana kivyovyote vile na jambo hili? (Ninadhani unahusiana kwa hali zote na jambo hili. Sasa Yesu amelipia na kurejesha kile alichokiumba wakati wa juma la uumbaji. Anakisherehekea kwa kupumzika. Wakristo wengi wanaiadhimisha siku ya Jumapili kwa sababu ni siku ambayo Yesu alifufuka kutoka kaburini. Wanakosea jambo la muhimu sana, maadhimisho ya pumziko la ushindi wa Yesu dhidi ya uovu.)
D. Soma Yohana 3:14-15 na Hesabu 21:8-9. Kwa nini Mungu anataka wadhambi waiangalie nyoka, kati ya vitu vyote wanavyoweza kuvitazama, ili waokolewe?
1. Kwa nini Yesu analinganishwa na nyoka wa hatari sana? (Nyoka anawakilisha dhambi. Yesu alikufa kwa ajili yetu. Alifanyika dhambi yeye asiyejua dhambi. 2 Wakorintho 5:21.)
E. Tafakari tena juu ya mjadala wetu wa awali kuhusu kafara ya kondoo na ujumbe alionao Mungu kwa ajili yetu. Nyoka kufananishwa na Yesu inatuambia nini juu ya umuhimu wa sheria? (Hii inahusu sisi kukabiliana na dhambi zetu. Kama sheria isingekuwa ya muhimu, basi kwenye kile kikao cha kuandaa msingi mbingu zingeamua tu kurekebisha sheria kwa namna fulani.)
F. Rafiki, msalaba unatufundisha upendo wa Mungu usiopimika, na unatufundisha umuhimu wa sheria. Je, utafanya uamuzi leo wa kuheshimu kile ambacho Yesu amekutendea kwa kuichukulia sheria yake na kafara yake kwa umakini mkubwa?
IV. Juma lijalo: Ushindi wa Kristo Dhidi ya Kifo.