Somo la 13: Viongozi Katika Yerusalemu
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mojawapo ya uwezo mkubwa ulionao lakini usiotambulika ni ushawishi. Tunapowafikiria viongozi wenye ushawihi, baadhi ya watu wanaweza kuchukulia kwamba watu fulani tu mahsusi wenye nguvu ndio wana uwezo wa kuwashawishi watu wengine. Imani yangu ni kwamba sote tuna aina fulani ya ushawishi kwa wengine. Je, kuna uzoefu wowote maishani mwako unaoweza kuukumbuka kwenye jambo ambalo mtu mwingine alilisema au kulitenda? Linaweza tu kuwa jambo moja, lakini ni lako. Tunapohitimisha somo letu la Ezra na Nehemia, hebu tuchimbue kile Biblia inachotufundisha kuhusu kuwashawishi watu wengine!
- Yosia
-
- Soma 2 Wafalme 22:1-2. Mtu mwenye umri wa miaka minane anaweza kuwa na ushawishi wa aina gani? (Mwanetu alipoanza kuongea alikuwa akivirejelea vitu vyote vizito kama “gonks.” Bado tunalitumia neno hilo nyumbani kwetu!)
-
- Mfalme Yosia, alipokuwa na umri wa miaka 26, aliamuru ukarabati wa hekalu. Hebu tusome 2 Wafalme 22:8. Kitu gani kinagundulika wakati wa ukarabati? (Biblia kama ilivyoonekana katika kipindi hicho.)
-
-
- Katika somo la 6 kwenye mfulilizo wa masomo yetu ya robo hii tulijifunza jambo kama hili katika Nehemia 8. Walisoma na kuifafanua Biblia kwa watu ambao hawakujua Biblia inazungumzia nini. Watu waliwezaje kuipoteza Biblia au kusahau kile Biblia ilichokizungumzia? (Kabla ya kipindi cha Yosia, Biblia ilipuuzwa. Katika kipindi cha Nehemia, taifa lilikuwa limevamiwa na watu kuchukuliwa mateka.)
-
-
- Soma 2 Wafalme 23:1-2. Tafakari mwelekeo wa ushawishi wa Yosia. Mungu anafanyaje kazi na Yosia ili kupanua wigo wake wa ushawishi? (Yosia anaanza na lengo la kawaida kabisa; kukarabati hekalu. Hii inasababisha kupatikana kwa Biblia. Sasa, Yosia anafanya Biblia isomwe mbele za watu.)
-
-
- Kuna fundisho lolote kwetu katika jambo hili? (Mwelekeo wetu wa kuwashawishi watu wengine katika hali chanya unaweza kuanza kwa njia rahisi kabisa. Mungu atabariki juhudi zetu.)
-
-
- Soma 2 Wafalme 23:3. Mfalme Yosia anafanya nini? (Anaahidi kumfuata Mungu na kuyatenda mapenzi yake “kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote.”)
-
-
- Hii inatoa ushawishi gani kwa watu? (Wanaahidi kufanya vivyo hivyo.)
-
-
-
- Yosia ana umri wa miaka 26 na ana ushawishi wa kweli wa jambo jema kwa taifa lake. Una ushawishi gani kwa wale wanaokuzunguka? (Nilipojiuliza swali hili miaka 35 iliyopita, ilinifanya nifanye mabadiliko makubwa maishani mwangu.)
-
- Nehemia
-
- Hebu tusome baadhi ya vifungu vinavyozungumzia kipindi ambacho Nehemia alikuwa anaongoza juhudi za kujenga upya ukuta katika Yerusalemu. Soma Nehemia 4:10-12. Watu wa Mungu wanasambaza ujumbe gani? (Hatuna nguvu za kutosha.)
-
-
- Ni nini ujumbe wa maadui wa Mungu? (Watawaua wafanyakazi pale wasipotarajia.)
-
-
-
- Kuna ujumbe gani kwa Wayahudi wanaoishi maeneo ya karibu? (Mashambulizi hayaepukiki.)
-
-
-
- Ni nini ulio ushawishi wa jumla wa ujumbe wote huu?
-
-
- Soma Nehemia 4:13-14. Nehemia anakabilianaje na huu ujumbe hasi? (Kwanza, anachukua hatua kuwalinda wafanyakazi dhidi ya shambulizi. Pili, anawatia moyo kwa kusema kuwa wanazipigania familia zao.)
-
-
- Je, unaweza kutumia njia hii kuongeza ushawishi wako?
-
-
- Soma Nehemia 2:10, Nehemia 4:7 na Nehemia 13:4-5. Hapo kabla tulijifunza suala la Eliashibu kutenga chumba hekaluni kwa ajili ya Tobia. Unamwelezeaje Tobia? (Yeye ni adui wa watu wa Mungu.)
-
-
- Soma Nehemia 13:6-9. Katika somo lililopita niliuliza kama Nehemia hakuwa na staha. Tulijadili endapo Nehemia alipaswa kumwambia Tobia kwa staha kuondoka badala ya kutupa nje vitu vyake vyote. Hapa Nehemia anaonyeshaje ushawishi wake? (Tobia ni mtu mbaya. Kama angeweza, hekalu lisingejengwa upya. Nehemia anachukua hatua madhubuti dhidi ya Tobia.)
-
-
-
- Je, wakati mwingine hatua madhubuti zinahitajika katika makanisa yetu leo? Je, wakati mwingine hii ndio njia sahihi ya kuonyesha ushawishi?
-
- Ezra
-
- Soma Ezra 7:8-10. Kwa nini “mkono mwema wa Mungu” ulikuwa pamoja na Ezra? (Alijitoa kujifunza, kuishika na kuifundisha sheria.)
-
- Soma Ezra 7:11-13. Sasa Ezra ana ushawishi wa namna gani? (Mfalme Artashasta amemwezesha Ezra kuwarudisha watu wa Mungu Yerusalemu. Hili ni mojawapo ya matukio ya muhimu kabisa katika historia ya watu wa Mungu na Ezra anaongoza juhudi katika kipindi hiki.)
-
- Soma Ezra 7:25. Sasa Ezra ana mamlaka gani makubwa ya kushawishi mambo yajayo? (Anawachagua na kuwafundisha waamuzi!)
-
-
- Kwa nini Ezra alichaguliwa kwa ajili ya jukumu hili la muhimu sana? (Uhusiano wake na Mungu. Mungu hakumpa Ezra hekima tu (Ezra 7:25), bali pia Ezra alijifunza na kuifundisha sheria.)
-
-
-
-
- Je, unaweza kuongeza ushawishi wako kwa kujifunza na kufundisha sheria ya Mungu? Au, je, unadhani hilo litakufanya upoteze ushawishi?
-
-
-
- Soma Ezra 7:27-28. Ni nini lengo la kazi ya Ezra? (Kuleta heshima katika nyumba ya Mungu.)
-
-
- Kitu gani kinamhamasisha Ezra kuamka asubuhi na kuifanya kazi yake? (Anapata ujasiri kutokana na ukweli kwamba Mungu yu pamoja naye.)
-
- Debora
-
- Soma Waamuzi 4:4-5. Debora alikuwa na wajibu gani katika Israeli? (Aliliongoza taifa. Alikuwa mwamuzi aliyetatua migogoro miongoni mwa watu. Alikuwa nabii.)
-
- Soma Waamuzi 4:6-7. Debora ana wajibu gani mwingine? (Anapokea mkakati wa kijeshi aliopewa na Mungu.)
-
- Soma Waamuzi 4:2-3. Sisera ana uwezo gani? (Magari yalikuwa ni teknolojia ya kisasa katika vita. Sisera ana magari 900 ya chuma!)
-
- Soma waamuzi 4:7. Mungu alimwambia Debora amwambie Baraka awapeleke watu wake mlimani. Kisha Mungu ataweka mpango wa magari 900 kuwa bonde. Je, kuna maelekezo yaliyoachwa kwenye ujumbe huu? (Ninataka kufahamu jinsi wanavyotumia nafasi yao mlimani kuyashambulia magari haya.)
-
- Soma Waamuzi 4:8. Baraka anayachukuliaje maelekezo haya? Baraka ana ushawishi wa namna gani kama kiongozi? (Ana hofu. Ushawishi wake utakuwa ni wa kueneza hofu.)
-
- Soma Waamuzi 4:9. Debora ana ushawishi gani kwa Baraka?
-
-
- Baraka anapunguzaje ushawishi wake?
-
-
-
- Tatizo la Baraka ni lipi? (Haamini kile alichoambiwa na Debora.)
-
-
-
-
- Kwa nini haamini? (Sidhani kama tatizo ni kuamini alichokisema Debora, nadhani tatizo la Baraka ni kumtumaini Mungu.)
-
-
-
-
- Je, kuna fundisho katika jambo hili linapokuja suala la ushawishi wetu? (Tukifanya mambo makubwa kwa kushirikiana na Mungu, itazidisha ushawishi wetu.)
-
-
- Hebu turuke mafungu kadhaa. Soma Waamuzi 4:13-15. Inamaanisha nini kusema kwamba “Bwana akamfadhaisha Sisera?” (Soma Waamuzi 5:20-22. Sasa tunafahamu jinsi kisichowezekana kilivyowezekana. Mto ambako magari yote yamekusanyika unabadilika kuwa damu.)
-
- Soma Waamuzi 4:17-20? Ni nani ambaye Sisera anahofia kwamba atakuja? (Baraka!)
-
- Soma Waamuzi 4:21-22. Nani anapata sifa kwa kumwua Sisera na nani anakosa sifa kama ilivyotabiriwa na Debora katika Waamuzi 4:9? (Baraka anapoteza heshima na mwanamke, Yaeli, anapata sifa/heshima.)
-
-
- Je, kuna fundisho kuhusu ushawishi kwenye kisa hiki? Je, kuna ujumbe kuhusu suala la kijinsia? Kwa nini Mungu aliweka kisa hiki kwenye Biblia? (Mada ya Biblia inayojirudiarudia ni kwamba Mungu anaegemea upande wa wanaume katika masuala ya uongozi. Licha ya mwegemeo huo, Mungu anamtumia mtu yeyote anayemwamini Yeye na kumtii bila woga. Nadhani hiyo ndio sababu ya kisa hiki. Kama mwanaume hatasimama, Mungu atawatumia wanawake kuushinda uovu.)
-
-
- Rafiki, una ushawishi wa aina gani kwa watu wengine? Kuwa mwaminifu, je, ushawishi huo ni mzuri au mbaya? Kama ni mbaya, au kama unaonekana kuwa ushawishi mdogo kwa jambo jema, kwa nini usidhamirie kutembea kwa ukaribu zaidi na Mungu ili uongeze ushawishi wako? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, akusaidie katika mwelekeo huo?
- Juma lijalo: Kristo: Kiini cha Danieli. Tunaanza mfululizo mpya juu ya kitabu cha Danieli.