Somo la 1: Kuifanya Historia Kuwa na Mantiki: Zerubabeli na Ezra
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Fikiria kwamba wewe ni raia wa Yerusalemu wakati Babeli inapouteka mji wako na kuangamiza hekalu lililojengwa na Mfalme Daudi na Mfalme Sulemani. Kunaweza kuwepo na jambo baya zaidi ya hili? Naam, ndiyo. Jambo baya zaidi ni kwamba katika Yeremia 25:11 Mungu anawaambia watu wake kuwa “nchi hii yote itakuwa ukiwa, nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa babeli miaka sabini.” Unaweza kubashiri pale utakapofia? Utumwani katika nchi ya ugeni. Tunaweza kujifunza nini kutokana na hiki kipindi kigumu? Hebu tuchimbue Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!
- Sikiliza
- Soma Yeremia 25:3-5. Mungu anawaahidi nini watu wake? (Kwamba wanaweza kuishi katika nchi yao milele.)
- Watu wa Mungu walitakiwa kufanya nini? (Kugeuka na kuacha tabia na matendo yao uovu.)
- Kifungu kinasema kuwa watu wa Mungu hawakuwa wasikivu. Unadhani kwa nini walishindwa kuwa wasikivu?
- Soma Yeremia 25:6-7. Kwa umahsusi, ni tabia zipi na matendo gani yaliyokuwa maovu kwa hawa watu wa Mungu? (Wanafuata miungu mingine. Hii ni miungu waliyoifanya kwa juhudi zao wenyewe.)
- Jiweke kwenye nafasi ya Mungu. Hii ni dhihaka kwa kiasi gani?
- Mustakabali
- Soma Yeremia 25:8-9. Unaona mantiki gani kwa Mungu kumfanya mfalme wa kipagani kuangamiza nchi ya watu wa Mungu? Je, inaendana na kukabiliana na dhambi? (Binafsi hii inaleta mantiki kwangu. Ikiwa watu wa Mungu watakitegemea kitu walichokitengeneza badala ya kutegemea uwezo wa Mungu, basi Mungu anasema, “Hebu tuone jinsi mtakavyofanya kwa uwezo wenu wenyewe?”)
- Kuna fundisho gani kwa ajili yetu leo? Tunaweza kutegemea kitu gani ambacho tumekitengeneza?
- Unadhani kwa nini Mungu anamwita Nebukadreza, mfalme wa kipagani, “mtumishi” wake?
- Robo iliyopita tulijifunza “Hawa Walio Wadogo.” Kuna maelekezo mengi kwenye Biblia kuhusu kubarikiwa ikiwa wewe ni mwaminifu na kulaaniwa ikiwa wewe si mwaminifu. Hali ambayo Yeremia anaiandikia inatufundisha nini? (Kwa upande mmoja inathibitisha kwamba utii huleta baraka. Lakini, inatoa onyo kwamba kwa kuwa tu tunadhani kwamba sisi ni watu wa Mungu waaminifu, tunaweza tusiwe sahihi. Tunaweza kuwa na tatizo katika kumsikiliza Mungu.)
- Utaona kwamba wapagani ambao hawajisingizii kumfuata Mungu wanawaangamiza watu wa Mungu. Hiyo inazungumzia nini kuhusu watu wabaya kulaaniwa?
- Soma Yeremia 25:11-12. Siku nyingi zijazo zina mustakabali gani? (Baada ya miaka 70 mwisho wa Babeli utafika. Wapagani wataadhibiwa. Kuna tumaini la siku zijazo. Kuna ahadi kwamba hatimaye wapagani hawatashinda katika kipindi kirefu kijacho.)
- Soma Danieli 9:1-2. Danieli ana uelewa gani juu ya unabii wa Yeremia ambao tumeusoma hivi punde? (Anauelewa kumaanisha kwamba adhabu itakuwepo kwa miaka 70 pekee.)
III. Kumtegemea Mungu
- Soma Danieli 9:3-6. Danieli anamwendeaje Mungu? Je, anazitumaini kazi zake? (Hapana. Daniel anaungama kwamba wameshindwa kusikiliza.)
- Soma Danieli 9:17-19. Unalichukuliaje ombi la Danieli kwa Mungu?
- Soma Danieli 9:20-23. Jibu linamfikia Daniel kwa haraka kiasi gani?
- Je, hii inaakisi muda wa safari kati ya dunia na mbingu?
- Soma Danieli 9:24-25. Gabrieli analeta habari gani njema? (Analeta habari njema nyingi, lakini tutajikita kwenye asili ya ombi la Danieli pekee – Yerusalemu itarejeshwa na kujengwa upya!)
IV. Marejeo
- Soma Ezra 4:1-2. Nini kimetokea? (Watu wa Mungu wamerejea Yerusalemu na wanaanza kujenga upya hekalu!)
- Je, si jambo jema unapohamia sehemu mpya na majirani wako wapya wanakupatia msaada?
- Kwa nini wakaazi waliopo wanataka kusaidia? (Wanasema kwamba wamekuwa wakimtolea dhabihu Mungu wa kweli tangu walipopelekwa mahali hapa.)
- Soma Ezra 4:3. Je, watu wa Mungu wanakuwa mafidhuli na wenye kuchukiza na karaha? Kwa nini kukataa msaada unaotolewa katika hali ya urafiki? (Hapa ndipo mambo yanapokuwa magumu. Wakaazi waliopo ni “Wasamaria,” watu wa Mataifa waliooleana na Wayahudi, watu wa Babeli hawakuwachukulia kuwa na hadhi ya kuwa watumwa wao. Kujitolea kwao kuwasaidia kunaweza kuwa kulihamasishwa na tamaa ya wao kuruhusiwa kuabudu kwenye hekalu jipya. Inaweza kuwa ilihamasishwa na tamaa ya kuwatawala Wayahudi wanaorejea.)
- Soma Ezra 4:4-6. Je, Wasamaria wanataka kulipiza kisasi kwa kuwa wamekataliwa? Au, je, hii inaonesha asili halisi ya kutaka kwao kusaidia? (Kama Wasamaria walitaka kumwabudu Mungu wa kweli, kama walitaka kuwa watu wa msaada, wasingechukua hizi hatua zote za kusimamisha ujenzi.)
- Hebu turukie mbele. Kama matokeo ya juhudi za Wasamaria, ujenzi upya wa hekalu unasimamishwa. Ezra sura ya 5 na 6 zinaandika mpambano wote wa kwenda mbele na kurudi nyuma juu ya ujenzi huu. Hatutaingia katika jambo hili kwa kina kwa sababu chanzo kimoja makinifu kinaeleza kwamba sura ya 5 na 6 zinachukua nafasi kabla ya kuandikwa kwa barua rasmi ya shutuma katika Ezra 4:6 na vifungu vinavyofuata.
- Soma Ezra 7:6 na Ezra 7:10-13. Hili ni tukio muhimu kiasi gani? (Mambo yanabadilika. Mfalme Artashasta, Mfalme wa Uajemi (Ezra 7:1), sasa ametoa amri kwamba Ezra na mtu yeyote anayejitolea anaweza kurejea Yerusalemu. Vizuizi kutoka kwa Artashasta sasa vimeondolewa. Furaha!)
- Je, umewahi kupitia uzoefu wa serikali kuwa kizuizi kwa ujenzi wa kanisa lako? (Tulipokuwa tunajenga kanisa, serikali ilikuwa chanzo cha wasiwasi mara kwa mara na ucheleweshaji. Tulipotaka kuboresha shule yetu ya kanisa, serikali ilisimamisha ujenzi na kamwe uboreshaji haukufanyika. Serikali ya mtaa kusababisha matatizo kwa ujenzi wa kanisa ilikuwa ni suala kubwa nchini Marekani, kiasi kwamba serikali ya shirikisho ilipitisha sheria kuyaruhusu makanisa kuishtaki serikali ya mtaa kwa kusababisha matatizo yasiyo na sababu.)
- Soma Ezra 7:15-16. Je, kuna jambo lolote baya na mtazamo wa Mungu kwa serikali kusaidia kuliunga mkono kanisa? (Msaada huu wa serikali unataarifiwa kwa idhini. Hakuna tatizo la kiteolojia kwa serikali kumrejeshea Mungu kile ambacho tayari ni chake.)
- Angalia jinsi Artashasta anavyomrejea Mungu wa Biblia. Je, anamkiri Mungu wa Israeli kuwa Mungu wa kweli dhidi ya miungu mingine yote? (Hapana. Lugha hii inaashiria kinyume chake. Rejea hii inaonekana kusema kwamba yeye ni Mungu wa nchi moja. Mungu anakaa Yerusalemu. Hii inaakisi mtazamo wa kale kwamba mungu alikuwa na mamlaka juu ya himaya fulani.)
- Je, ukweli kwamba Artashasta si muumini ni tatizo kwa kukubali msaada kutoka kwake? (Kwa mara nyingine, Mungu ni mtawala juu ya vyote. Ukweli kwamba wapagani wanatangaza ufalme wa Mungu si tatizo. Ndio namna ambayo maisha yanavyopaswa kuwa.)
- Soma Ezra 7:21-23. Kitu gani kinamhamasisha Artashasta kuwa mkarimu sana kwa Ezra na Mungu wa Mbinguni? (Ana wasiwasi kuhusu ghadhabu ya Mungu kumshukia yeye pamoja na wanaye.)
- Hebu tuliangalie jambo hili kwa kina zaidi. Je, ni tatizo kwamba serikali inaunga mkono mpango wa Mungu kutokana na hofu? Je, msaada unapaswa kujengwa juu ya upendo? (Kile ambacho Wakristo wengi wanakihofia ni kuliunganisha kanisa na dola ili kukomesha uhuru wa dini kwa ajili ya mtazamo wa wachache. Kuwa na serikali inayofanya kazi kutokana na hofu ya Mungu huenda ni jambo jema. Inawezekana ni salama zaidi kuliko kuwa na serikali inayopenda dini fulani mahsusi na kujaribu kutekeleza matendo yake ya kidini.)
- Rafiki, je, unakabiliana na matatizo maishani? Je, ulimwengu wako umepinduliwa juu chini, na “watu wabaya” wameingia madarakani? Uwe na amani kwenye uelewa wa kwamba Mungu anadhibiti mambo yote. Je, utamtumaini Mungu juu ya mustakabali wako?
V. Juma lijalo: Nehemia.