Pambano la Kiulimwengu
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Wikendi iliyopita nilipokuwa nikiendesha gari barabarani, nilikuwa ninazingatia kile ambacho dereva mwingine alikuwa akikifanya kwenye msitari wa pili wa magari barabarani. Matendo yake yalisababisha mnyororo wa matukio yaliyoishia kuniathiri. Nilimwambia mke wangu kuwa ninajaribu kuyaangalia kwa makini magari yote yanayonizunguka barabarani. Alinijibu kuwa binti yetu wa kwanza alipoanza kuendesha gari, kwa uchache sana alizingatia uelekeo aliokuwa akiendesha. Vipi kuhusu wewe? Unapokuwa unaendesha gari, je, unataka kujua kile kinachoendelea katika mazingira yanayokuzunguka barabarani? Vipi kuhusu maisha? Je, ungependa kufahamu “taswira pana” ya kile kinachoendelea kwenye mazingira yako katika dunia na ulimwengu? Hilo ndilo lengo la mfululizo mpya wa masomo yetu. Tulifikaje hapa tulipo? Matukio gani ya kiulimwengu yanatanabaisha mustakabali wetu? Tupo mahala gani katika historia? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
- Kuibuka kwa Uovu
-
- Soma Isaya 14:12. Mtu huyu aliyeangushwa alianguka kutoka wapi? (Mbinguni!)
-
- Soma Ezekieli 28:14. Huyu “kerubi mlinzi” anatembea wapi? (Katika “mlima mtakatifu wa Mungu.”)
-
-
- Endapo ungefuatilia mwanzoni mwa sura ya kitabu cha Isaya (hususani Isaya 14:4) ungeona kuwa inazungumzia “Mfalme wa Babeli.” Ukifuatilia mwanzoni mwa sura ya 28 katika kitabu cha Ezekieli (hususani Ezekieli 28:12) utaona inamzungumzia “Mfalme wa Tiro.” Je, inaonekana kuwa na mantiki kwamba ama Mfalme wa Tiro au Mfalme wa Babeli walikuwa mbinguni au walitoka mbinguni? (Hawa wafalme wa kidunia kamwe hawakuwa mbinguni. Badala yake, tunapaswa kuelewa jambo hili kama tunavyouelewa ujumbe wa Yesu katika Mathato 24. Hapo, Yesu alielezea mambo mawili tofauti (ujio wake wa Mara ya Pili na kuangamizwa kwa Yerusalemu) bila kuyatenganisha kwa wasikilizaji wake. Katika kitabu cha Isaya na Ezekieli tunazo rejea za wanadamu na pia mtu mwingine.)
-
-
- Soma Ezekieli 28:15-17. Nini kilimtokea huyu “kerubi mlinzi” aliyeishi katika “mlima wa Mungu?” (“Alifukuzwa” na Mungu “akamtupa chini (duniani).”)
-
- Soma Ufunuo 12:7-9. Kifungu hiki kinasema kuwa nani “aliyetupwa katika nchi?” (Shetani. Maelezo haya hayana utata.)
-
- Tunapolinganisha Ufunuo 12:7-9 na Isaya 14:12 na Ezekieli 28:17 tunaona taswira ya Shetani kufukuzwa mbinguni. Inaleta mantiki kuhitimisha kwamba vitabu vyote vitatu vinazungumzia tukio moja. Hebu turejee kwenye kitabu cha Isaya na tuchambue jambo hili zaidi. Soma Isaya 14:13. Unauelezeaje mtazamo wa Shetani alipokuwa mbinguni? (Alikuwa na zaidi ya tamaa ya makuu. Alitaka kuzitawala (“nitakiinua kiti changu”) “nyota za Mungu.”)
-
-
- Unadhani “nyota za Mungu” ni zipi? Soma Ufunuo 12:4, Ufunuo 1:20 na Ayubu 38:7. (Vifungu hivi vinazungumzia malaika na yumkini viumbe wengine walioumbwa kule mbinguni. Shetani alitamani kutawala angalao malaika wote.)
-
-
- Soma tena Ezekieli 28:16-17. Tunaona tabia gani hapa? (Shetani alikuwa na vurugu na alijivunia mwonekano wake na akili na umahiri wake. Majivuno haya yaliharibu fikra zake.)
-
- Soma Isaya 14:14. Shetani alitaka jambo gani jingine? (Kufaana na Mungu!)
-
- Soma Mwanzo 3:1-5. Jambo gani liko katikati ya hili jaribu la Eva? (Kwamba “atafanana na Mungu.”)
-
- Kutokana na kile tulichojifunza hadi kufikia hapa, unadhani dhambi iliibukaje mbinguni? (Kiburi/majivuno. Kutoridhika. Tamaa ya kuwa kiongozi, kufanana na Mungu, kuwa Mungu. Shetani alipomjaribu Eva, alitumia kigezo kile kile kilichomsababishia anguko.)
-
-
- Utaona kwamba wote wawili, yaani Shetani na Eva, walikuwa wakamilifu waliposhindwa kishawishi (jaribu) hiki. Hiyo inakuambia nini?
-
-
- Dhambi gani, jaribu gani unalopaswa kulizingatia zaidi leo? Ikiwa unao huu mtazamo mpana wa pambano kati ya Mungu na Shetani, tatizo gani linalopaswa kukufanya ukae macho usiku? (Kuanguka kwenye kishawishi cha kutaka kufanana na Mungu. Dhambi ya kiburi.)
-
-
- Soma Mwanzo 1:26-28. Mungu aliwaumbaje wanadamu? (Ili wafanane naye. Kutawala uumbaji.)
-
-
-
- Kwa dhahiri huu ni wito wa utambuzi! Ni mahali gani tunapochora msitari kati ya jaribu la siri lenye madhara makubwa sana na kufanya kazi ambayo Mungu alituumba ili tuifanye? (Kuvuka msitari ni suala linalotia changamoto mahali petu hapa duniani. Dhambi inakuwa mtawala wetu mdogo kinyume na matakwa yetu. Kamwe hatutakiwi kufanya wajibu zaidi ya ule ambao Mungu ametupatia na kujaribu kufanana na Mungu kwa maana ya kuchukua nafasi yake.)
-
-
-
- Hebu tuwe mahsusi zaidi kwa sasa. Unaona dhambi gani zinazoakisi mtazamo wa kuchukua wajibu wa Mungu? Kunyakua/kutwaa nafasi ya Mungu? Kutomtii Mungu kama mtawala wa vitu vyote? (Kutoamini kwamba Mungu yupo! Kutoamini kile Biblia inachokisema kuhusu vitu kama vile mwanzo wa wanadamu, dhambi ni nini, na nini kisicho dhambi. Kudai wajibu wa Mungu na kuwa hakimu wa watu wengine.)
-
- Kazi ya Mwovu
-
- Soma Ufunuo 12:7-9. Shetani na malaika wake walioanguka wapo wapi sasa hivi? (Wapo katika maeneo yetu! Wametupwa chini duniani.)
-
- Hebu tuangalie msingi wa vifungu hivi. Soma Ufunuo 12:1-4. “Joka kubwa jekundu” inaonekana kuwa rejea nyingine ya Shetani kupoteza nafasi yake mbinguni na kuchukua theluthi ya malaika pamoja naye. Unadhani mwanamke ni nani?
-
- Soma Ufunuo 12:5-6. Mtoto ni nani? (Hii itakuwa inamzungumzia Yesu. Yeye ndiye mtoto aliyezaliwa duniani ambaye “atawachunga (atatawala) mataifa yote” na ambaye “alinyakuliwa hata kwa Mungu na kwa kiti chake cha enzi.”)
-
-
- Je, hii inamfafanua “mwanamke?” (Mariamu alimzaa Yesu. Mariamu na Yusufu walikimbilia Misri baada ya kuzaliwa kwa Yesu (Mathayo 2:13-15). Lakini, hapa ishara inaonekana kwenda zaidi ya Mariamu na kurejea (kuzungumzia) kanisa la Mungu.)
-
-
-
- Hebu turuke vifungu vichache chini ili tupate ufafanuzi wa maana ya mwanamke. Soma Ufunuo 12:17. Sasa unaelewaje ishara ya mwanamke? (Kwa dhahiri kabisa hii inakwenda zaidi ya Mariamu, na ni ufafanuzi wa kanisa la kweli.)
-
-
- Sasa tunaelewa maana ya joka, mtoto, na mwanamke. Soma Ufunuo 12:13-17. Kazi ya sasa ya mwovu ni ipi? (Kufanya vita dhidi ya kanisa, wafuasi wa Yesu.)
-
- Angalia tena Ufunuo 12:17. Unajuaje kama wewe ni mlengwa wa Shetani? Unajuaje kama wewe ni sehemu ya kanisa la kweli? (“Wale wazishikao amri za Mungu na kuwa na ushuhuda wa Yesu.”)
-
-
- Hebu tuone kama tunaweza kulinyumbulisha jambo hili zaidi. Inamaanisha nini kung’ang’ania kwenye “ushuhuda wa Yesu?” (Soma Ufunuo 1:9. Yohana, ambaye aliandika kitabu cha Ufunuo, anasema kuwa yupo kwenye kisiwa hiki “kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu.” Yohana anazungumzia juu ya kazi yake ya kuwaambia watu wengine habari za kwamba Yesu ni Mungu. Wale wanaoandamwa na Shetani ni wale wanaoitangaza injili ya Yesu.)
-
-
-
- Unadhani inamaanisha nini kuzishika amri za Mungu? (Shetani anakulenga wewe ikiwa unaishi maisha ya kumtii Mungu.)
-
-
-
- Hebu tuangalie jambo moja zaidi ambalo Yohana analisema kuhusu ushuhuda wa Yesu. Soma Ufunuo 19:9-10. Hapa kasoro ya Yohana ni ipi? (Kujaribu kumwabudu malaika.)
-
-
-
-
- Malaika anasema kuwa Yohana (pamoja na sisi) anapaswa kumwabudu nani ikiwa tunatangaza “ushuhuda wa Yesu?” (Mungu. Roho Mtakatifu ndio nguvu iliyo nyuma ya ushuhuda wetu kwa Yesu. Tunatakiwa kuhakikisha kuwa hadhira yetu inaelekezwa kwa Mungu, na si kuelekezwa kwetu au kwa mtu yeyote yule.)
-
-
- Kazi ya Mungu
-
- Soma Mathayo 28:18-20. Ikiwa tunatenda kile anachokiamuru Yesu, tutalengwa na Shetani. Jambo gani linalopaswa kutuliwaza na kutupatia hakikisho? (Yesu atakuwa pamoja nasi siku zote – hata “ukamilifu wa dahari.”)
-
- Soma Ufunuo 14:8. Jambo gani jingine linalopaswa kutuliwaza tunapotenda kazi ya Yesu? (Yesu anashinda. Yesu ameshinda. Babeli imeanguka!)
-
- Rafiki, yatafakari maisha yako. Unajihusishaje na majivuno yako? Unapoyatafakari mafundisho ya Biblia, je, unayapuuza baadhi ya mafundisho kwa sababu ya ujuaji wako (kwamba una ufahamu zaidi)? Ikiwa ndivyo, unatakiwa kutubu leo juu ya huu mtazamo wa Kishetani. Kwa nini usifanye uamuzi sasa hivi kuungana na wale wanaotangaza injili ya Yesu na kuzishika amri zake?
- Juma lijalo: Danieli na Wakati wa Mwisho.