Hakuna Hukumu
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Hebu kwanza tupitie fundisho la Paulo kidogo. Katika Warumi 5 Paulo anatuambia kuwa tunapewa uzima wa milele kama matokeo ya maisha, kifo na ufufuo wa Yesu. Kisha katika Warumi 6, Paulo anaelezea kuwa hii karama ya neema haimaanishi kwamba tuendelee tu kutenda dhambi. Kwa kuwa tu tumeifia sheria, hatupewi leseni ya kutenda dhambi. Halafu katika Warumi 7, Paulo anatufundisha kuwa ingawa tunapaswa kuchagua kuepuka dhambi, yeye mwenyewe anaendelea kupambana na asili yake ya dhambi, nasi tutarajie kufanya vivyo hivyo. Mwisho, tunaingia kwenye somo letu la juma hili. Hata kama mapambano yetu dhidi ya dhambi ni jambo halisi, Paulo anatuambia kuwa ikiwa tuko ndani ya Yesu, “hakuna hukumu.” Hebu tuzame kwenye some letu kuhusu hili hakikisho la pekee!
- Hakuna Hukumu
-
- Soma Warumi 8:1-2. Tumewekwa huru dhidi ya nini? (“Sheria ya dhambi na mauti.”)
-
-
- Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Ili kuwa na uhakika kwamba tunaelewa muktadha, soma Warumi 7:21-25. Hatuko tena chini ya sheria isemayo kuwa kama tunatenda dhambi (na sote tunatenda dhambi) tutakufa kifo cha milele.)
-
-
- Soma Warumi 8:3. Kwa nini Yesu alifanya hivi kwa ajili yetu? (Tusingeweza kufanya hivyo. Amri Kumi “hazikuwa na uwezo” kutokana na asili yetu ya dhambi. Tusingeweza kuishika sheria na kuupata wokovu.)
-
-
- Utaona kwamba kifungu hiki kinaishia na maneno, “na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili.” Inamaanisha nini kusema kuwa Yesu aliihukumu dhambi kwa matendo yake kwa ajili yetu? (Kamwe tatizo halikuwa sheria. Tatizo ni asili yetu ya dhambi. Yesu hataki tujichafue dhambini. Anahukumu dhambi maishani mwetu. Lakini, anatupatia njia ya kutoka ili tusiingie kwenye mauti ya milele.)
-
-
- Soma Warumi 8:4. Matakwa ya sheria yanafikiwaje maishani mwetu? (Kwa njia ya Yesu. Kile ambacho kamwe tusingeweza kukifanya, alikufa kwa ajili yetu.)
-
-
- Sehemu ya mwisho ya kifungu hiki inataabisha. Inaonekana kuiweka neema kwenye vigezo vya kutoishi kwa mujibu wa asili yetu ya dhambi. Tunawezaje kutoishi kwa mujibu wa asili ya dhambi wakati Paulo ameendelea kusisitiza kuwa asili yetu ya dhambi ndio tatizo, na si sheria? (Hii inaturejesha kwenye uchaguzi wetu. Asili yetu ya dhambi ipo siku zote. Lakini Mungu anatuita tufanye uchaguzi wa kuishi kwa mujibu wa Roho wake, na si kwa mujibu wa asili yetu ya dhambi. Tunapokea neema tunapoichagua neema ya Mungu na Roho wa Mungu.)
-
- Kuyafikiri Mambo ya Mwili
-
- Soma Warumi 8:5. Utakumbuka kwamba katika Warumi 7:14-16 Paulo anatuambia kuwa anatenda kile asichopenda kukifanya. Kile anachotaka kukifanya hakitendi. Unadhani kuwa Paulo, anapoandika mambo haya, mawazo yake yamejikita kwenye jambo sahihi? (Ndiyo. Ikiwa Paulo hakuyaweka mawazo yake katika kutenda mambo ambayo Yesu alimtaka ayafanye, kamwe asingeandika mambo kama vile “sikutenda kile nilichotaka kukitenda, nilitenda kile ambacho sikutaka kukifanya.” Badala yake, Paulo anaandika kuwa alifanya kile ambacho hasa alidhamiria kukifanya, na kile ambacho asili yake ya dhambi ilimtaka akifanye.)
-
-
- Mara nyingi katika siku za nyuma nimeandika kuhusu “haki kwa njia ya mtazamo.” Paulo anapoandika katika Warumi 8:5 kuhusu kuyafikiri mambo ya mwili, je, hazungumzii mtazamo wetu?
-
-
-
- Una udhibiti wa kiasi gani juu ya mtazamo wako? (Hii inaturejesha kwenye kazi ya Roho Mtakatifu. Unaweza kufanya uchaguzi. Lazima ufanye uchaguzi. Lakini, kile unachokichagua ni kuishi kwa mujibu wa mwongozo wa Roho Mtakatifu, na si kwa mujibu wa asili yako ya dhambi. Hata wale wanaochagua kuishi kwa mujibu wa mwongozo wa Roho Mtakatifu wanagundua kwamba si mara zote matendo yao yanaendana na mapenzi yao. Soma tena Warumi 7:21-25 ili kuelewa kikamilifu hali inayotukabili.)
-
-
- Soma Warumi 8:6. Sote tuna asili ya dhambi. Paulo anamaanisha nini anapoandika “nia ya mwili (mdhambi) ni mauti?” (Kwa mara nyingine hii inarejea (inazungumzia) chaguzi za mitazamo. Je, tutachagua kufuata asili yetu ya dhambi na kuongozwa nayo, au tutachagua kumfuata Roho Mtakatifu na kuongozwa naye?
-
- Soma Warumi 8:7. Kuna hatari gani hapa? (Kumpendeza Mungu. Kumpa Mungu utukufu.)
-
- Soma Warumi 8:8. Unadhani inamaanisha nini “kudhibitiwa na asili ya dhambi?” Tulipojifunza katika Warumi 7 kwamba Paulo alifanya mambo ambayo hakutaka kuyatenda, je, hiyo haioneshi kuwa “alidhibitiwa” na asili yake ya dhambi? (Kujihusisha na vitendo vya dhambi visivyoendana na mapenzi yetu ya kumpendeza Mungu haimaanishi kuwa tunadhibitiwa na asili yetu ya dhambi. Tafsiri nyingine zinatumia neno “in the realm of the flesh.” Dhana iliyopo ni kwamba mtazamo wetu ni kuchagua asili yetu ya dhambi.)
- Roho Mtakatifu
-
- Soma Warumi 8:9. Je, hii inasaidia kujibu swali la awali juu ya kile kinachomaanishwa “kudhibitiwa” na asili yetu ya dhambi? (Ndiyo! Kwa kweli hii ni habari njema sana. Ikiwa unataka Roho Mtakatifu akae ndani yako, na una uhakika kuwa Roho Mtakatifu anakaa ndani yako, basi “haudhibitiwi” na asili yako ya dhambi.)
-
-
- Ni muhimu kiasi gani kuwa na Roho Mtakatifu akaaye ndani yako? (Paulo anatuambia kuwa kama hatunaye Roho Mtakatifu, basi sisi si wa Yesu. Hili ni jambo zito sana, na ni faraja kuu. Ni zito kwa sababu hatujaichagua neema ikiwa Roho Mtakatifu hayumo maishani mwetu. Kwa upande mwingine, ikiwa tumemkaribisha Roho Mtakatifu, na tunamwona akitenda kazi maishani mwetu, basi hatuna haja ya kuwa na mashaka juu ya yule anayetudhibiti.)
-
-
- Soma Warumi 8:10-11. Je, hii inaonekana kama mtu aliye huru dhidi ya dhambi? (Kifungu kinasema kuwa “mwili wetu umekufa kwa sababu ya dhambi.” Lakini, Roho Mtakatifu anatupatia uzima. Kama Roho Mtakatifu alivyomfufua Yesu kutoka kifoni, wale waliompokea Yesu kama mbadala wao pia watafufuliwa katika uzima wa milele!)
- Tunapaswa Kuishije?
-
- Soma Warumi 8:12-13. Wajibu wetu unatokana na nini? (Tafakari jambo hili. Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Alitupatia zawadi kubwa sana; ushindi dhidi ya dhambi. Tunawajibika kupambana na dhambi inayoendelea kututesa na kutuumiza. Tunao ushindi, kwa nini basi tutake kugaagaa dhambini?)
-
-
- Je, tupo peke yetu kwenye haya mapambano? (Hapana. Roho Mtakatifu yule yule atupatiaye uzima wa milele ataifanya dhambi ife (ikome) maishani mwetu.)
-
-
- Soma Warumi 8:14. Je, umewahi kutafakari hapo kabla umuhimu wa Roho Mtakatifu kukaa ndani yako? (Sisi ni watoto wa Mungu ikiwa tunaye Roho Mtakatifu maishani mwetu!)
-
- Soma Warumi 8:15. Tunazungumzia hofu ya aina gani hapa? (Je, umegundua kwamba maisha yako yalipokuwa yanadhibitiwa na asili yako ya dhambi ulikuwa na wasiwasi juu ya matokeo ya maamuzi yako ya dhambi? Ulipungukiwa amani? Kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu hutupatia amani na furaha.)
-
-
- Je, kuna jambo la ziada zaidi ya kuepuka tu matatizo yanayosababishwa na dhambi? (Ikiwa Roho Mtakatifu anaweza kukupatia uzima wa milele, ikiwa Roho Mtakatifu anaweza kukuongoza katika kuepuka dhambi, kama mtoto wa Mungu tafakari nguvu iliyopo kwa ajili yako! Tafakari mtazamo wa Mungu dhidi yako. Unawezaje kuwa na hofu?
-
-
- Soma Warumi 8:16. Roho yako ni ipi? Baadhi ya watu wanafundisha kwamba “roho” ya wanadamu ni pumzi ya Mungu tu. (Angalia Mwanzo 2:7.) Je, fundisho la “pumzi” linaleta mantiki katika muktadha wa Warumi 8:16? (Roho Mtakatifu anawasiliana na sehemu ya mwili wetu inayohusika na kufikiri kwamba yeye yupo maishani mwetu.)
-
-
- Je, umewahi kupitia uzoefu huu? Kwamba mawazo yako yanafahamu kuwa Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani yako?
-
-
- Soma Warumi 8:17. Katika vifungu kadhaa vinavyofuatia, Paulo anajadili dhana ya mateso kwa kina zaidi. Mateso yanaonekana kuibuka kutokana na mapambano yetu na dhambi. Je, mapambano dhidi ya dhambi maishani mwetu (kutenda yale tusiyotaka kuyatenda) yanaweza kuwa chanzo cha mateso? (Tafakari kwamba Yesu alijizuia (aliepuka) dhambi maishani mwake. Tunapewa wito wa kuendelea na mapambano hayo.)
-
- Rafiki, habari njema ni kwamba unaokolewa kwa neema pekee ikiwa utachagua kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu. Pia ni habari njema kwamba Roho Mtakatifu atakusaidia kuishi maisha yanayokuletea mibaraka na kumpa Mungu utukufu. Kwa nini usidhihirishe tena sasa hivi kwamba unamchagua Mungu?
- Juma lijalo: Watoto wa Ahadi.