Tabia ya Ayubu
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Ayubu alikuwa shujaa wa Mungu. Kwenye pambano kati ya wema na uovu, Mungu alimteua Ayubu kama mpambanaji wake kwenye mpambano baina yake na Shetani. Kichekesho ni kwamba, Shetani alijichagua yeye mwenyewe kuwa mpambanaji katika timu yake. Je, jambo hili linakukumbusha juu ya mtu mwingine katika Biblia? Vipi kuhusu Adamu na Eva? Wao ndio waliokuwa kiini katika pambano kati ya Mungu na Shetani. Vipi kuhusu Yesu? Mara hii Mungu anajichagua yeye mwenyewe, lakini akiwa katika mfumo wa mwanadamu, kuwa Mshindi kwa ajili ya wema. Je, umewahi kufikiria kama wewe ni mpambanaji wa Mungu? Je, inajalisha, kwenye pambano kati ya wema na uovu, endapo unafanikiwa kama Ayubu na Yesu, au unashindwa kama Adamu na Eva? Nadhani jambo hili ni la msingi na linahusika kwa hali ya juu. Juma hili tutaangalia jinsi Ayubu alivyoishi ili tuone mambo tunayoweza kujifunza juu ya namna ya kuwa washindi wa Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!
I. Mitazamo Sahihi ya Ayubu
A. Soma Ayubu 1:1. Kifungu hiki kinazungumzia mambo manne kumhusu Ayubu. Ni mkamilifu, mwelekevu, mcha Mungu, na aliepukana na uovu. Je, mambo haya yote manne yanamaanisha kitu kimoja? Au, je, unaona tofauti katika mambo hayo? (Ninaona tofauti katika huu msamiati wote. “Ukamilifu” inaonekana kuzungumzia kwamba usingeweza kuona dosari kwa Ayubu. “Uelekevu” inamaanisha kwamba Ayubu alitenda kilicho sahihi.)
1. Wakati ukamilifu na uelekevu vina kufanana kwingi, unadhani inamaanisha nini, kivitendo, “kumcha Mungu?” (“Kumcha” Mungu kunarejea suala la mtazamo: kumheshimu na kumstahi Mungu. Huenda pia inamaanisha kuwa na uelewa wa kwamba Mungu anao mpango bora zaidi kwa ajili ya ulimwengu na kwa ajili yetu.)
2. Je, hii ni tofauti na “kuepukana na uovu?” (Wakati watu wengi wanafahamu kuwa Mungu ana mpango kamili kwa ajili ya maisha yao, bado wanajikuta wanavutwa uovuni.)
a. Je, hiki ndicho kinachoendelea maishani mwako? Katika maeneo ambayo una udhaifu kwa dhambi kujipenyeza, je, unajichorea msitari, na kisha unaukaribia sana msitari huo huku ukiwa na wazo kwamba hutauvuka? (Hiki ni kinyume tu cha “kuepukana” na uovu.)
B. Soma Ayubu 1:8. Je, unataka kuwa mtu bora zaidi? Je, kuna baadhi ya maeneo maishani mwako ambapo ungependa kusema, “Hakuna aliye bora zaidi kunishinda katika eneo hili?” Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu nafasi ya Ayubu? (“Hapana mmoja aliye kama yeye duniani” katika vigezo tulivyovijadili: mkamilifu, mwelekevu, mcha kumcha Mungu na mwenye kuepukana na uovu.)
1. Kuishi maisha yenye tabia hizi kunafananaje? Hebu tugeukie jambo hili katika sehemu inayofuata.
II. Matendo Sahihi ya Ayubu
A. Soma Ayubu 29:11-12. Tunawaona watu masikini kila mahali wakituzunguka. Biblia haifundishi kwamba kila mtu anatakiwa kuwa na vitu (mali) sawa. Badala yake, Biblia inaashiria kwamba maskini wanaweza kuwa na faida kiroho (Yakobo 2:5) na inafundisha kwamba Wakristo wanapaswa kujifunza kuridhika na vitu walivyonavyo (Wafilipi 4:12, Waebrania 13:5). Ayubu anawachaguaje maskini wa kuwasaidia? (Anamsaidia maskini “anayemlilia” na anamsaidia yatima “asiyekuwa na mtu wa kumsaidia.”)
1. Hivi karibuni nilipokuwa ninatoka dukani, kijana mmoja mdogo aliniambia kuwa atakapotoka kazini atakwenda kushiriki kwenye “matendo ya huruma bila utaratibu/mpango maalum.” Nikamuuliza, “Kwa nini uende mahali popote bila kuwa na mpango maalum? Kwa nini usidhamirie kutenda jambo maalum?”
a. Je, Ayubu “hakuwa na utaratibu maalum” katika matendo yake ya huruma? (Sidhani. Tunaona kwamba alikuwa na mkakati. Aliwasaidia wale waliomwomba kwa dhati (“waliomlilia”), na aliwasaidia wale ambao hawakuwa na mtu wa kuwasaidia.)
B. Soma Ayubu 29:13. Huu ni msaada wa aina gani?
1. Mtu anayekaribia kufa atakuwa na hitaji gani kuu? (Kinyume na ukweli kwamba anaelekea kufa, atajali sana mustakabali wa familia yake. Na katika muktadha huu, mkewe.)
2. Kwa nini moyo wa mjane unaimba wakati mumewe anafariki? (Unapoifikiria hali hii, ni dhahiri kwamba Ayubu anaandaa mipangilio ya namna fulani hivi ili kuhakikisha kuwa mjane ataweza kusaidiwa. Nabashiri kwamba Ayubu anampa kazi kwenye biashara yake.)
C. Soma Ayubu 29:16-17. Ayubu anavichukuliaje vitendo visivyo vya haki? (Anachukua hatua kuvikomesha.)
1. Ayubu anachukua hatua gani mahsusi? (Anamsaidia “mtu asiyemjua” – mtu ambaye katika hali ya kawaida hana marafiki mahakamani. Anawaokoa waathirika wa waovu.)
2. Je, unashangaa kwamba Ayubu anazivunja taya za waovu? Hii inamaanisha nini? Kwamba anawapiga ngumi za mdomoni watu wabaya? (Tafsiri ya Biblia yangu inasema kuwa Ayubu anavunja “shina la jino” la waovu. Kwa nyoka, jino lenye sumu ndio njia ya kupitishia sumu. Nadhani Ayubu anazivunja njia ambazo waovu wanazitumia kutenda uovu wao.)
a. Chukulia kwamba wewe ni Ayubu wa zama za leo. Je, ungetimizaje jambo hilo leo? (Nchini Marekani, serikali ama inafadhili au inalazimisha mifuko inayoendeleza uovu kufanya hivyo. “Kuvunja mashina ya meno” ya mashirika haya ni kujaribu kuondoa ufadhili wao.)
D. Soma Ayubu 31:1. Hatujui Ayubu aliishi zama zipi, lakini kwa dhahiri ilikuwa kabla Yesu hajaelezea mtazamo wake mpana juu ya uzinzi katika Mathayo 5:27-28. Linganisha Mathayo 5:28 na Ayubu 31:1 kisha uniambie kama unadhani Yesu na Ayubu wanamaanisha kitu kimoja?
1. Yesu anaposema kuwa mwanaume anayemwangalia mwanamke kwa kumtamani “amekwisha kuzini naye moyoni mwake,” unadhani kauli ya “moyoni mwake” inamaanisha nini? (Nimeelewa inamaanisha kwamba ikiwa mwanaume alitaka kuzini na mwanamke, lakini hakuweza kufanya hivyo kutokana na sababu fulani, dhambi ya kiakili tayari imeshafanywa. Bila kujali kama mwanaume (au mwanamke) ana fursa hiyo au la haileti tofauti yoyote.)
E. Soma Ayubu 31:1-3. Ujumbe wa jumla wa Ayubu ni upi katika vifungu hivi? (Mungu atawaangamiza waovu.)
1. Ikiwa mtu anaendeleza azma/tamaa yake ya kufanya ngono na mtu asiye mwenzi wake, je, kitendo hicho kitasababisha uangamivu kwa mtu huyo katika dunia hii? (Kutoka 20:17 inatuamuru tusimtamani mwenzi wa mtu mwingine. Muktadha unaashiria kwamba Ayubu na Yesu kwa namna fulani hivi wanazungumzia mambo tofauti. Ayubu anajikita kwenye suala la kumtamani mtu asiye mwenzi wako. Yesu anazungumzia uamuzi wa kuzini, endapo itawezekana. Kwa kuwa Ayubu anatuambia kuwa Mungu anawazia kuwaangamiza wasio watiifu, anasema “Nimedhamiria kutochukua hatua ya kutokutii kwa kutomwangalia mwanamke kwa tamaa ya kuzini naye.”)
F. Hebu turuke mafungu kadhaa kwa sababu Ayubu anarudia mada hii. Soma Ayubu 31:9-10. Je, hapa Ayubu anazungumzia dhambi itendwayo mawazoni? (Wakati ambapo jambo hili haliko wazi sana, rejea yake ya wanaume wengine kulala na mkewe inaashiria asili ya dhambi anayoijadili – kufanya uzinifu kivitendo.)
G. Soma Ayubu 31:11-12. Ayubu anasema kwamba matokeo ya uzinifu ni yapi? (Anasema kuwa ni “moto uteketezao hata Uharibifu,” “fedheha,” na jambo “litakalong’oa maongeo [mavuno] yangu yote.” Hii ni dhambi yenye matokeo mabaya ya muda mrefu, dhambi inayoondoa maanani mambo mazuri ambayo mtu anaweza kuwa ameyatenda hapo awali.)
H. Soma Ayubu 31:5-6. Ni kwa namna gani nyingine ambayo Ayubu amekuwa mtiifu kwa Mungu? (Yeye ni mwaminifu. Sio kawaida yake kufanya vitendo visivyo vya uaminifu (“kutembea katika ubatili”), na haendekezi kuwadanganya watu wengine (“kuukimbilia udanganyifu”).)
I. Soma Ayubu 31:13-15. Ni kwa namna gani nyingine Ayubu ni mwaminifu kwa Mungu? (Kwa namna anavyowatendea watu wanaomfanyia kazi.)
1. Je, unatakiwa kuwa mwajiri ili dhana hii iweze kutumika? (Hapana. Mtu yeyote aliye chini ya udhibiti wako, hata kama ni kwa muda mfupi tu, ana haki ya “kutendewa haki.” Hii inawajumuisha watu walio chini yako kazini kwako, au wale wanaokutumikia kwa namna moja au nyingine, kama vile mtumishi katika mkahawa.
2. Sababu ya kuwatendea haki wale walio chini ya mamlaka yako ni ipi? (Nyote mko sawa mbele ya Mungu.)
J. Rafiki, unapotafakari maeneo haya maishani mwako, unajilinganishaje na Ayubu? Pamoja na kwamba tunaokolewa kwa neema pekee, na sio kwa matendo yetu, sisi ni “wapambanaji” kwenye pambano kati ya wema na uovu, na matendo yetu yana athari kwa watu wengine. Je, utadhamiria sasa hivi, kwamba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu uishi maisha yanayomuakisi Mungu na kuwa na athari chanya kwa watu wengine?
III. Juma lijalo: Mambo ya Kujifunza Kutoka kwa Ayubu.