Haki na Rehema Katika Agano la Kale: Sehemu ya 2
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Unapotafakari kazi ya Roho Mtakatifu katika Biblia, je, unajikita zaidi katika Agano Jipya? Je, unaweza kuboresha fikra hiyo zaidi, kwa kusema kwamba msisitizo juu ya Roho Mtakatifu unaanzia kwenye kitabu cha Matendo? Juma hili tunapata mwangaza zaidi kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu katika Agano la Kale! Tafakari jambo hilo. Hebu tuzame kwenye uchunguzi wetu wa kitabu cha Agano la Kale juu ya kile ambacho Roho Mtakatifu anashughulika nacho kuhusu haki na rehema maishani mwetu!
1) Mifupa
a) Soma Ezekieli 37:1. Hebu tutafakari jambo hili mawazoni mwetu. Mungu anamsafirisha Ezekieli kwenye safari ya kweli (katika roho) angani na kumtuisha katika bonde lililojaa mifupa. Ungemwambia nini Mungu endapo angekufanyia hivyo? (Tungeweza kutua mahali pengine tafadhali? Mahala hapa panaonekana kama sehemu ya mauaji.)
b) Soma Ezekieli 37:2-3. Unalichukuliaje jibu la Ezekieli kwa Mungu? (Jibu zuri sana!)
c) Soma Ezekieli 37:4-6. Je, swali hili ni la mtego? Je, Mungu anamtania Ezekieli? (Hapana. Mungu anamfundisha Ezekieli jambo fulani.)
i) Hebu tuone kama tunaweza kutambua fundisho la Mungu. Mifupa inamaanisha nini? (Watu wasio hai.)
ii) Jambo gani linaanzisha ufufuaji wa hii mifupa? (Kwanza Ezekieli anazungumza maneno ya kiunabii kutoka kwa Mungu. Hii inafuatiwa na mifupa kulisikia neno la Mungu.)
iii) Jambo gani linaifanya mifupa kuwa hai tena? (Mungu kuipulizia hewa ya uhai.)
d) Soma Ezekieli 37:7-10. Hatua zote ni za muhimu, lakini je, Mungu anajikita kwenye hatua ipi ambayo ni ya muhimu zaidi? (Pumzi ya Mungu kuiingia mifupa.)
e) Unawezaje kutumia jambo hili maishani leo? Unajifunza nini kutokana na jambo hili kwa washiriki wa kanisa (yumkini makanisa yote) ambao ni “mifupa iliyokauka?” (Kwanza, panatakiwa pawepo na juhudi za makusudi (unabii) za kuwasilisha neno la Mungu ili waweze kulisikia. Pili, Mungu anapulizia juhudi zetu pumzi yake ili kuleta uhai.)
i) Unadhani “pumzi ya Mungu” ni kitu gani? (Roho Mtakatifu. Ingawa mara nyingi Roho Mtakatifu anawasilishwa kama moto, katika Matendo 2:2-3 anawasilishwa kama moto na upepo. Hii inaendana na wazo la Mungu kupulizia Roho yake kwenye hii mifupa.)
ii) Ikiwa tutakuwa na mfanano kama huo leo, kuna umuhimu gani zaidi kuwarejeshea uhai washiriki wa kanisa waliokauka na kuyafufua makanisa yaliyokauka? (Roho Mtakatifu!)
f) Soma Ezekieli 37:11-14. Kulikuwa na fundisho gani kwa watu wa zama za Ezekieli? (Kwamba Mungu atawafufua/atawafanya upya watu wake. Kwa mahsusi katika jambo hili fungu linasema “nitatia roho yangu ndani yenu nanyi mtaishi.” Utaona kwamba jambo la dhahiri linatimilika – watu wanakaa kwenye ardhi/nchi yao.)
g) Maisha yako yakoje? Uhai wa kanisa lako ukoje? Je, una ile hisia ya “mifupa iliyokauka?” Au, je, unamwona Roho Mtakatifu maishani mwako na kanisani kwako?
i) Je, mambo haya yanahusianaje na haki na rehema? (Mifupa ya Ezekieli ilipata uhai na kukaa katika ardhi/nchi yao; ikimaanisha kuwa walitenda jambo fulani. Roho Mtakatifu anapotujaa na kukaa ndani yetu, nasi pia tunaweza kutenda mambo ambayo Mungu ameyaandaa kwa ajili yetu.)
2) Maji ya Chumvi
a) Soma Ezekieli 47:1-6. Taswira hii inatofautianaje na ile ya mifupa? (Hili ni tatizo la unyevunyevu na maji, sio ukavu.)
i) Maji yote haya yanatokea wapi? (Hekalu la Mungu.)
b) Soma Ezekieli 47:7-9 na Ezekieli 47:12. Maji haya yanaleta nini? (Uhai. Maji ya chumvi yanaua baadhi ya vitu, maji baridi (“maji matamu”) huleta uhai.)
c) Angalia maono ya mifupa iliyokauka na haya maono ya maji. Je, Mungu anawaambia watu wake jambo lile lile kwa namna tofauti? Au, je, unaona tofauti halisi katika haya maono mawili tofauti? (Lengo la Roho Mtakatifu ni kuifanya mifupa mikavu iwe na “majimaji.” Tulichokipata mwishoni mwa maono ya mifupa ni “jeshi kubwa.” Hii inaifanya ionekane kwamba “unyevu” unaotoka hekaluni ni watu wa Mungu. Watu hao ni maji baridi na yanayasukuma maji ya chumvi yanayoua mimea na wanyama. “Unyevu” unaonekana kuwa ni kanisa lililopo kazini lililovuviwa Roho Mtakatifu.)
i) Unadhani kwa nini maji katika maono ya Ezekieli yalianza kwa kiasi kidogo sana na kuishia kuwa mto mkubwa? (Mungu anatutaka tujue kwamba kazi yake ni endelevu. Tunaweza kuanza katika hali ya chini sana, lakini kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, watu wa Mungu watakuwa na nguvu kubwa kabisa.)
3) Roho Mtakatifu Kazini
a) Soma Isaya 61:1. Kutokana na utangulizi wa habari za mifupa na maji, unalielewaje fungu hili? (Roho Mtakatifu anatuwezesha kuwapelekea injili wale ambao hawaenendi vizuri kwa sababu hawamjui Mungu. Hawa ndio “waliovunjwa moyo,” “mateka” na “wafungwa” wa giza la Shetani. Sisi ambao ni “mifupa mikavu” tunawezeshwa na Roho kufanya kazi ya “kunyevusha” kwa kuwapelekea injili na kuyabadilisha maisha ya watu hawa!)
b) Soma Isaya 61:2. Je, tuna ujumbe mchanganyiko? (Upendeleo na kisasi ni vitu viwili vinavyokinzana.)
i) Ni kwa jinsi gani upendeleo na kisasi huwafariji wale wanaoomboleza?
c) Hetu tutafakari jambo hili kwa dakika chache. Utakumbuka kwamba waliovunjika moyo, mateka na wafungwa wanasaidiwa. Hapo awali walijeruhiwaje? (Maana yake ni kwamba walijeruhiwa na Shetani na wale wanaomfuata (wafuasi wake).)
i) Kisasi kinawezaje kuliwaza? (Habari njema ya Mungu ni kwamba anatoa haki kwa watenda makosa na uhuru na ufariji kwa wale waliotendewa makosa. Waliotendewa makosa wanaamini kuwa haki imetendeka.)
d) Soma Isaya 61:5-6. Lengo la watu wa Mungu ni lipi? (Wageni watafanya kazi za hadhi ya chini (kulisha mifugo) na kazi ngumu za mikono (kulima). Kwa upande mwingine, watu wa Mungu watajihusisha na uongozi wa dini na kutajirika kutokana na kazi za mataifa mengine.)
i) Wow! Je, ulifahamu kwamba Biblia inasema hivyo?
e) Soma tena Isaya 61:1. Fungu hili linaleta mantiki gani kwako? Tunaanza kwa habari njema kwa “maskini,” na habari hizo ni kwamba watawekwa huru, wataponywa, na kukaa katika nchi ili kwamba wageni waweze kuwatumikia! Je, hiyo inaleta mantiki? Kumbuka tunajadili jinsi Roho Mtakatifu atakavyotuchangamsha ili tujishughulishe kwenye matendo ya haki na rehema.
i) Je, matendo ya haki na rehema ni kwa ajili ya maskini na sio matakwa ya jumla kwa ajili ya watu wote wa ulimwengu huu?
ii) Ulijifunza nini kwenye somo la juma lililopita kuhusu Mungu anavyowahudumia maskini? (Takribani katika maeneo yote walitakiwa kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia chakula. Wajane kanisani waliokuwa wakipewa msaada wa mara kwa mara walitakiwa kuwa na historia ya kutenda mambo mazuri. Unaweza kuona kwamba mfululizo wa mantiki inayojitokeza kwenye mambo yote haya ni kwamba Mungu haangalii namna ya kuwasaidia maskini wote, bali anaangalia namna ya kuwasaidia maskini wenye haki. Hiyo inaweza kuelezea Isaya 61:1 ambayo inawabainisha maskini wa aina fulani kwa ajili ya kuwasaidia.)
f) Soma Luka 10:27-29. Mtaalam wa sheria anamwuliza Yesu swali gani? (Swali lile lile ambalo tunalijadili – jirani yangu maskini ni yupi ambaye ninapaswa kumsaidia? Je, hawa ni watu wema tu?)
g) Soma Luka 10:30-37. Je, Msamaria alijaribisha ustahili au haki ya mtu aliyepigwa na kujeruhiwa? (Hapana.)
i) Je, ushauri wa Yesu kwa mtaalam wa sheria unakinzana na ushauri wa Agano la Kale linapokuja suala la matendo ya sheria na haki? (Hapana. Ninaona utofauti mkubwa kwenye kisa cha Msamaria Mwema. Hii ni hali ya dharura. Tunapaswa kuwasaidia watu wote yanapokuja masuala ya dharura na magumu ya muda mfupi. Lakini, yanapokuja masuala ya muda mrefu, tunaelekezwa kutumia fedha zetu na muda wetu kuuendeleza Ufalme wa Mungu katika maisha ya mtu anayehitaji msaada.)
h) Soma Luka 15:17-20. Hiki ni kisa cha Mwana Mpotevu. Alipokuwa kwenye mateso, je, kukosa msaada kulimsababishia nini huyu kijana mdogo? (Kulimfanya arejee kwenye ufahamu wake. Hii inaelezea aina ya maamuzi ambayo Mungu anayataka kutoka kwetu. Tunapaswa kuwasaidia maskini wenye haki. Kwa maskini wasio na haki, msaada wetu unatakiwa kutangaza heshima na mibaraka ya kazi. Tunatakiwa kuangalia matumizi bora ya fedha zetu. Tunatakiwa kuwasaidia wasio na haki kurejea kwenye ufahamu wao.)
i) Rafiki, ikiwa wewe ni “mfupa uliokauka,” linapokuja suala la haki na rehema, je, utamwomba Roho Mtakatifu akuchangamshe ili uwasaidie watu wengine kwa namna inayoendana na hekima ya Kibiblia, na sio tu matendo holela ya huruma/wema?
4)Juma lijalo: Yesu Katika Utandaaji kwa Jamii.