Urejeshwaji wa Mambo Yote
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mungu anashambuliwa! Uadilifu wa Mungu na mamlaka yake kama Muumbaji, Mbunifu na Mkombozi vimedhoofishwa na Shetani tangu mwanzo kabisa. Shambulizi linaendelea hadi leo. Swali kwa kila mwanadamu ni “Je, unafanya wajibu gani katika pambano kati ya wema na uovu?” Somo letu la Biblia juma hili linatusaidia kuelewa vizuri masuala haya. Hebu tuchimbue na kujifunza zaidi!
1) Kupoteza Sura/Mfano wa Mungu
a) Soma Mwanzo 1:26-27. Chukulia kwamba hujawahi kabisa kuyasoma mafungu haya. Je, unajifunza nini kutokana na mafungu haya? (Tunaishi kwa sababu Mungu alituumba. Mungu aliwaumba wanadamu wawe watawala wa vitu vyote vilivyoumbwa na aliwaumba wanadamu kwa sura na mfano wake. Mungu aliwaumba wanadamu, mwanaume na mwanamke – na hiyo inaakisi sura na mfano wake.)
i) Kwa kuwa somo letu linahusu “urejeshwaji,” je, mambo mangapi uliyojifunza kwenye mafungu haya yametiwa doa, kama si kuangamizwa, na Shetani? (Dhana maarufu inayoendelea hapa duniani inasema kuwa wanadamu walitokana na uibukaji, na kwamba hawakuumbwa. Hawakuanza kwa “sura,” achilia mbali mfano wa Mungu. Dhana maarufu inasema kwamba wanadamu wanautumikia uumbwaji na si uumbwaji kumtumikia mwanadamu. Dhana maarufu inasema kwamba kufanana kwa mwanaume na mwanamke sio jambo la muhimu.)
ii) Miongo kadhaa iliyopita niliamua “kujifanyia tathmini,” ili kutathmini ushawishi wangu. Sikuyapenda matokeo. Unawezaje kufikia hatua ya kujifanyia tathmini kuhusu mpango wa asili wa Mungu? Je, ushawishi wako upo kwa wale wanaovunjavunja mpango wa asili wa Mungu?
b) Soma Mwanzo 3:1-5. Umuhimu wa jaribu la Eva ni upi? (Kutomwamini Mungu.)
i) Wafikirie wale wanaokubaliana na dhana ya uibukaji, wanamazingira waliokubuhu, na ndoa za jinsia moja. Unawalinganishaje na Eva? (Kwa dhahiri hawamwamini Mungu au wanadhani kuwa mpango wa Mungu si wa muhimu.)
ii) Soma tena Mwanzo 1:27. Je, masuala haya sio ya msingi tena siku hizi? (Mungu anasema kuwa mambo haya yanaakisi sura yake. Kuifuta sura/mfano wa Mungu duniani ni kinyume na kile ambacho Mkristo anatakiwa kuwa anakifanya.)
c) Soma tena Mwanzo 3:4-5. Tunaamini kuwa Mungu habadiliki, je, Shetani pia habadiliki? Je, Shetani anatumia mbinu zile zile leo kama alivyofanya dhidi ya Eva – kutomwamini Mungu?
i) Je, wewe na mimi tunapaswa kufanya nini kuhusu jambo hilo? Je, tunapaswa kukaa kimya?
(1) Endapo ungekuwepo wakati nyoka anamjaribu Eva, je, ungekaa kimya?
d) Soma Mwanzo 3:22-24 na 1 Yohana 2:1-2. Mungu aliwafanyaje wale ambao hawakumwamini? (Mungu aliwafukuza kutoka Edeni ili wasije wakala matunda ya Mti wa Uzima. Lakini, Mungu pia aliweka mpango wake wa wokovu kwa wale waliotenda dhambi kwa kutomwamini.)
2) Kuipata Sura/Mfano wa Mungu
a) Soma Wagalatia 3:6-7. Jambo gani ni la muhimu katika kuhesabiwa haki? (Kumwamini Mungu. Eva hakumwamini Mungu.)
b) Soma Wagalatia 3:10-12. Wagalatia walionywa dhidi ya jambo gani? (Dhidi ya kuitegemea torati kwa ajili ya wokovu wao.)
i) Soma Mambo ya Walawi 18:5. Utagundua kwamba Paulo ananukuu fungu hili kwenye Mambo ya Walawi. Inamaanisha nini? (Torati inafanya mambo mengi sana mazuri. Kuitii sheria kunatusaidia kuishi maisha ya furaha zaidi. Kuitii sheria humpa Mungu heshima na pia hutupatia heshima. Lakini, kuitii sheria hakutuokoi.)
c) Soma Wagalatia 3:13-14. Jambo gani linatukomboa katika laana ya torati? Jambo gani linatupatia wokovu? (Yesu. Imani katika maisha, kifo na ufufuo wa Yesu kwa ajili yetu.)
d) Soma Wagalatia 3:21-25. Kuna uhusiano gani kati ya torati na imani kwa Yesu? (Torati ni nzuri, inatuelekeza kuyaishi maisha bora. Hata hivyo, sisi ni wadhambi, na kujaribu kuitii sheria kunatufundisha kwamba hatuwezi kuishika/kuitii sheria kikamilifu.)
e) Hebu tutafakari jambo hili kidogo. Unailinganishaje dhambi ya Eva na dhambi ya Wagalatia? (Hii ni mirengo miwili inayotofautiana kabisa tunayoiona kanisani leo. Kuna wale wanaojiita wafuasi wa Yesu ambao hawaamini anachokisema Mungu kuhusu uumbaji, uhusiano wetu na uumbaji, na wajibu wa kijinsia katika mahusiano ya wanadamu kimapenzi (kingono). Katika upande mwingine wapo wanaojiita Wakristo ambao hawaelewi kwamba wajibu wa sheria ni kuboresha maisha yako, sio kuthibitisha stahili yetu ya wokovu. Makundi yote mawili yanashindwa kumweka Yesu kwenye nafasi yake sahihi maishani mwetu.)
3) Wajibu wa Kanisa Katika Urejeshwaji
a) Soma 1 Wakorintho 12:12-13. Tumejadili pande hizi mbili zinazotofautiana kabisa – kutomwamini Mungu na kuitegemea torati kwa ajili ya wokovu. Tuna ulinzi gani kutokana na dosari hizi? (Kuwa sehemu ya mwili wa Kristo – ambao ni kanisa.)
i) Kwa nini kuwepo na huo ulinzi dhidi ya dosari? (Soma 1 Wakorintho 12:7-10. Kama jinsi ilivyo dosari kuamini kwamba tunaweza kujiokoa kwa matendo yetu, vivyo hivyo ni kosa kuamini kuwa tunaweza kuifanya kazi ya Mungu kwa uwezo wetu.)
b) Soma 1 Wakorintho 12:11. Jambo gani linatumika kama kiunganishi kanisani? (Roho Mtakatifu. Kwa mara nyingine tena tunarejea kwenye suala la kutomwamini Mungu. Yesu alituambia kuwa Mungu atampeleka Roho Mtakatifu kutufundisha (Yohana 14:26).)
c) Soma 1 Wakorintho 12:14-20. Roho Mtakatifu anafanya uchaguzi gani katika kuliendesha kanisa? (Kila mmoja wetu ni mshirika katika mwili mkubwa wa kanisa. Hizi ni juhudi za pamoja, sio juhudi za mtu mmoja mmoja.)
i) Je, umegundua kwamba watu ambao wamejitenga na kuwa kwenye upande mmoja wenye mrengo tofauti kwa ujumla huwa wanafanya kazi peke yao au wanafanya kazi na kundi dogo? (Faida ya kundi kubwa ni kwamba linasaidia kuepuka dosari.)
4) Juhudi Katika Kundi
a) Soma Marko 2:1-3. Walihitajika watu wangapi kumbeba mtu mwenye kupooza?
b) Soma Marko 2:4. Walihitajika watu wangapi kufanya uamuzi wa kumbeba mtu mwenye kupooza kupitia darini kwa kutoboa dari ili kumfikia Yesu?
c) Soma Marko 2:5. Nani ambaye ni “yao” katika kauli ya “Yesu alipoiona imani yao?” (Kwa dhahiri, ni wale watu watano.)
d) Hebu tutafakari sehemu ya kisa tulichokisoma hadi sasa. Je, ungejisikiaje kama ungekuwa Yesu ukijaribu kufundisha kundi la watu na kundi jingine linatoboa dari juu yako? (Ningeudhika sana kutokana na huo uvurugaji wa utulivu, lakini Yesu anaangalia mambo yote hayo na kuiita “imani.”)
i) Je, yule mtu mwenye kupooza angeweza kuyafanya yote hayo peke yake? (Kwa dhahiri, hapana.)
ii) Unadhani kwa uchache wangehitajika watu wangapi kutimiza kazi ya kumfikisha huyu mtu kwa Yesu? Je, haya ndio mahesabu tunayotakiwa kuyafanya tunapokuwa na kazi ya utume?
e) Soma Marko 2:5. Unadhani hiki ndicho ambacho wale watu watano walitaka kukisikia?
i) Endapo ungekuwa mmojawapo wa wale watu watano na ukatafakari mambo uliyoyafanya siku hiyo, je, ungesema kuwa siku yako imekuwa ya kukatisha tamaa? Kwanza kundi la watu, kisha kupanda juu ya dari, halafu kutoboa tundu kubwa, kisha kumwomba Yesu msaada. Baada ya yote hayo, Yesu anasema jambo lisilo sahihi!
f) Soma Marko 2:6-7. Tuchukulie kwamba watu hawa watano wanawakilisha kazi iliyoratibiwa na kanisa. Je, mara zote mambo huwa yanafanyika kama kundi la kanisa linavyofikiria?
i) Kwa nini Yesu hasemi mara moja jambo la wazi kabisa, “Inuka uende zako?” (Yesu anayo taswira pana mawazoni mwake. Jambo hili halimhusu tu mtu mwenye kupooza. Jambo hili pia linawahusu viongozi wa dini na wote wanaotazama.)
g) Soma Marko 2:8-12. Jambo gani limetimizwa kwa hili tukio la imani lililotekelezwa na kundi la watu watano? (Kwanza, mtu wao aliyepooza ameponywa. Pili, dhambi zake zimesamehewa. Tatu, Yesu analidhihirishia kundi lililokusanyika kwamba yeye ni Mungu, na anayo mamlaka ya kusamehe dhambi na kuponya! Imekuwa siku njema na ya pekee sana!)
h) Rafiki, je, ulifanya uamuzi kwamba ushawishiwako si ule ambao ungepaswa kuwa? Ikiwa hivyo ndivyo, kwa nini usidhamirie leo kumtumaini Mungu na kwa uongozi wa Roho Mtakatifu ukatafuta kundi kwa ajili ya kuuendeleza Ufalme wa Mungu?
5)Juma lijalo: Urejeshwaji wa Mamlaka.