Vita Vinavyoonekana na Visivyoonekana
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Wakristo wengi wana mojawapo kati ya maoni ya aina mbili yanayokinzana. Wanadhani kwamba wokovu unatokana na matendo yao mema, au wanadhani kuwa wokovu ni suala tu la kuipokea na kuikubali neema na kisha kuendelea na mambo yao ya kawaida. Somo letu juma hili linabainisha njia ya tatu: kumtegemea Mungu katika kila jambo. Hii haijumuishi wokovu pekee, bali pia inajumuisha matatizo yote na ushindi wote unaopatikana maishani. Hebu tuchimbue somo letu la Mathayo ili tujifunze zaidi!
I. Mashaka ya Yohana
A. Soma Mathayo 11:1-3 na usome Mathayo 3:11-14. Kimetokea nini katika imani ya Yohana kwa Yesu? (Soma Mathayo 14:3-4. Yohana yupo gerezani wakati anawatuma wanafunzi wake kwa Yesu. Ukiangalia tena Mathayo 3:12 Yohana anatabiri kwamba Yesu “atayateketeza kwa moto usiozimika.” Pamoja na hayo, licha ya matarajio ya Yohana ya uwezo mkuu, Yesu hafanyi chochote kumtoa gerezani. Mathayo 14:10 inatuambia kuwa Yohana alifia gerezani.)
1. Hii inatufundisha nini kuhusu kuwa na majigambo juu ya namna tunayodhani kuwa unabii utatimizwa? (Tunatakiwa kuwa macho (makini) na kuyaweka mawazo yetu wazi kwa ajili ya kumpokea Roho Mtakatifu. Taifa la Kiyahudi (hii ikiwa ni pamoja na Yohana Mbatizaji) lilitarajia kuwa Yesu angetumia mamlaka na kuwaangusha maadui wake katika kipindi hicho.)
B. Soma Mathayo 11:4-6. Hili linajibuje swali la Yohana kuhusu sababu inayomfanya Yesu asimwokoe Yohana? (Jibu la Yesu linaonesha kwamba anamshinda Shetani, na sio wafuasi wa Shetani. Tunatakiwa kukumbuka kwamba adui halisi ni Shetani na nguvu zake za kishetani, sio watu ambao tunafanya nao kazi na kuishi nao.)
C. Soma Mathayo 11:7-11. Yesu anawezaje kusema kuwa hakuna mwanadamu aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji, pamoja na hayo, aliye mdogo katika ufalme wa Mbinguni ni mkuu kuliko Yohana?
1. Wanafunzi wa Yohana waliibua suala gani? (Yesu ni nani? Hilo ndilo suala la msingi maishani. Je, utamwamini Yesu na kumtumaini pamoja na matatizo na changamoto zako zote? Yohana alikuwa anadhihirisha upungufu wa imani. Watakaokwenda mbinguni watafika huko kutokana na kumtumaini Mungu – sio kutokana na matendo yao.)
2. Hii inatufundisha nini kuhusu kumtegemea Yesu badala ya kujitegemea wewe mwenyewe, kuwategemea wanadamu wengine au kuzitegemea fedha? (Hata Yohana Mbatizaji alitetereka. Tunatakiwa kuwa makini.
II. Vita
A. Soma Mathayo 11:12-14. Watu hawa wenye nguvu ni akina nani? (Angalia muktadha. Yohana Mbatizaji alitenda matendo makuu ili kumwandalia Yesu njia. Alikuwa “Eliya.” Lakini, Herode alimwua Yohana. (Mathayo 14:6-11.) Shetani huleta uwezo wa kibinadamu dhidi ya kanisa pale kanisa linapokuwa linasitawi.
B. Soma Mathayo 11:16-19. Hii inatuambia nini kuhusu kuwa na matarajio potofu? (Sisi, kama ilivyo kwa watoto, tunadhani kuwa watumishi wa Mungu wanapaswa kukubaliana na mawazo yetu. Tuna ubinafsi. Yesu anasema angalia mbali zaidi ya mawazo yako na uangalie anachokitenda Mungu kupitia kwa huyo mtu. Angalia jinsi Mungu anavyotamalaki ulimwenguni – hata ikiwa ni matokeo ya watu ambao hawafikii matarajio yako.)
1. Unawafahamu Wakristo wangapi wanaogombana, badala ya kushindana na nguvu za kishetani?
C. Soma Mathayo 11:20-24. Tunaifikiria Sodoma kwa kuihusianisha na dhambi ya zinaa. Yesu anasema kuwa jambo baya kuliko hilo ni lipi? (Kuipuuzia miujiza ambayo Mungu ametutendea maishani mwetu. Mfikirie tena Samsoni. Mtu huyu alikuwa na tatizo la zinaa. Licha ya hayo ameorodheshwa kwenye orodha ya mashujaa wa imani (Waebrania 11:32) kwa sababu hata katika dakika chache za mwisho wa uhai wake alimtumaini Mungu (Waamuzi 16:28-30).)
1. Je, haujaizingatia sana miujiza ambayo Mungu amekutendea maishani mwako?
D. Soma Mathayo 11:25-26. Muda mfupi uliopita Yesu alikuwa anawakosoa wasikilizaji wake kwa kuwafananisha na “watoto wanaokaa sokoni” (Mathayo 11:16) na sasa anasema Mungu anawafunulia “watoto wadogo” mambo waliyofichwa “wenye hekima na akili.” Tufanye nini sasa, je, tunapaswa kuwa na mtazamo kama wa watoto au la? Ni jambo gani basi, lenye kufanana na mtazamo wa watoto, ambalo Yesu analipendekeza kwetu? (Katika maeneo yote mawili Yesu anawaita watoto kuwa “wasio na makuu.” Hawana makuu kwa yale wanayoyataka na hawana makuu katika uelewa wao.)
1. Kwa nini jambo hilo ni jema? (Yesu anaonekana kumaanisha kuwa wito wa injili unaweza kueleweka na mtu yeyote ili mradi tu mtu huyo hana majigambo makubwa sana kiasi cha kutokuwa radhi kuipokea injili.)
2. Unadhani Mungu anamficha injili mtu yeyote? Kwamba kuficha habari njema ni kwa ajili ya “starehe” ya Mungu? (Ingekuwa vigumu kuelezea kazi kubwa ya Mtume Paulo endapo ingekuwa kweli kwamba Mungu aliwaficha injili “wenye hekima na akili”)
3. Soma Mathayo 19:23-24. Kwa nini ni vigumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni? (Hii inasaidia kufafanua tatizo la uelewa wa injili kwa “wenye hekima na akili.” Matajiri, werevu, na watu walioelimika sana wana jambo lenye kufanana, ambalo ni kuutegemea utajiri, kuitegemea akili na elimu badala ya kumtegemea Mungu. Hiki ndicho kile kile ambacho Yesu alikisema kwa Yohana Mbatizaji. Suala la msingi kwa Yohana lilikuwa ni endapo atamtumaini Mungu katikati ya matatizo. Suala la msingi kwa matajiri, wenye hekima na wasomi ni endapo watamtumaini Mungu au watazitumaini fedha zao, maarifa yao au elimu yao.)
E. Hebu turejee nyuma na tusome Mathayo 11:15. Nani awezaye kuuelewa ujumbe wa Yesu? (Kila mwenye masikio!)
1. Hilo linatuambia nini kuhusu maoni ya Yesu juu ya injili kufichwa kwa watu wa aina fulani? (Hii inasaidia kuthibitisha kwamba sote tunaweza kusikia na kuelewa, labda kama tutachagua kutokuelewa kwa sababu ya majivuno yetu na kujitegemea wenyewe.)
F. Soma Mathayo 11:27. Mungu amemfunulia nani injili? (Amemfunulia Yesu! Yesu anamfunua Mungu Baba kwetu. Hii inakazia alichokisema Yesu kwamba tunatakiwa kumtumaini yeye, tunatakiwa kumtegemea yeye.)
G. Soma Mathayo 11:28-30. Tunapata faida gani kwa kumtumaini Yesu? (Anabeba mizigo yetu. Anatupumzisha. Yeye si mkali wala hatutendei vibaya. Badala yake, anataka tufanikiwe maishani na kuwa na uzima wa milele.)
1. Je, unahisi kwamba maisha ni mapambano yasiyokoma? Kwa nini usimtegemee Yesu kwa kila jambo?
2. Unadhani kumtegemea Yesu kunafananishwa na jambo gani kivitendo? (Kunahusisha angalao mambo matatu. Kwanza, kumwomba Yesu kwa njia ya maombi kushughulikia changamoto zetu. Pili, kufuata ushauri ambao tayari Yesu ametupatia kwenye Biblia. Tatu, kumtazama Roho Mtakatifu atuongoze kwenye maamuzi tunayoyafanya.)
H. Soma Mathayo 12:24. Jambo gani ni baya zaidi ya kujitegemea wewe mwenyewe, badala ya kumtegemea Yesu? (Kudhani kwamba Yesu anamtegemea Shetani.)
I. Soma Mathayo 12:25-26. Unalifikiriaje jibu hili? (Hili ni jibu halisia sana kivitendo. Nadhani Yesu anashindana na tatizo ambalo amelibainisha, kwamba watu wanaojitegemea wenyewe wamefichwa ukweli.)
1. Jibu gani litakuwa sahihi kwa wale wanaomtegemea Yesu? (Kuna vita vinavyoendelea kati ya Yesu na Shetani. Kwa nini Shetani amsaidie Yesu? Lengo lake ni kumwangamiza Yesu.)
J. Soma Mathayo 12:27-28. Unadhani viongozi wa dini ya Kiyahudi walidhani kuwa viongozi wengine wa dini ya kiyahudi waliondoa pepo kwa uwezo wa Shetani? (Hapana! Yesu anasema “Kwa nini mnihukumu kwa kutumia viwango tofauti?”)
K. Soma Mathayo 12:29. Hii inatuambia nini kuhusu uhalisia wa pepo? (Inatuambia kuwa sio tu kwamba Yesu anawaamini, bali pia anamwita Shetani “mtu mwenye nguvu.”)
1. Hii inatuambia nini kuhusu Yesu? (Ana nguvu kuliko Shetani. Anaweza kumfunga Shetani.)
L. Soma Mathayo 12:30-32. Kuna hatari gani kusema kuwa Mkristo mwenzako anafanya uponyaji kwa uwezo wa Shetani? (Hii ni hatari sana.)
M. Rafiki, unao uchaguzi wa kufanya. Je, utaishi maisha yako ukimtumaini Yesu? Au, utaishi maisha yako huku ukijitegemea mwenyewe, au kibaya zaidi, kuzitegemea nguvu za Shetani? Yesu anajitolea kubeba mizigo yetu na kutupumzisha. Kwa nini usikubali ofa yake sasa hivi?
III. Juma lijalo: Pumziko Ndani ya Kristo.