Ndugu Katika Umoja
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unatenganisha kazi yako na masuala ya kidini? Baadhi ya watu wanadhani kuwa hivi ni vitu viwili tofauti maishani. Nilipokuwa chuoni, nilifanya kazi kidogo kwenye kiwanda cha kutengeneza matela ya malori katika lizizo ya majira ya joto. Wafanyakazi wenzangu walininyanyasa kutokana na “uanafunzi wangu” pamoja na imani zangu za kidini. Mwishoni mwa majira ya joto, kiongozi wa wafanyakazi alinijia na kuniomba msamaha kutokana na manyanyaso hayo. Aliniambia kuwa yeye alikuwa mwalimu wa “Sunday School” na kwamba kile alichokuwa akiniambia hakiendani na wajibu na majukumu yake kanisani. Biblia inatufundisha kuwa tunatakiwa kufungamanisha kazi yetu na imani yetu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone jinsi tunavyoweza kuwa “Ndugu Katika Umoja” hata katika mahali pa kazi!
- Weledi wa Petro
- Soma Luka 5:1-3. Kutokana na uzoefu wako wa matumizi ya mitumwi, je, wazo la Yesu kwamba afundishe akiwa chomboni linaibua matatizo yoyote? (Mtumbwi si chombo chenye utuli (kisichosogeasogea) isipokuwa tu kama kitatiwa nanga kadhaa. Nahisi Petro pia alikuwa ndani ya chombo akitumia kasia kukifanya chombo kiwe mahali pamoja.)
- Soma Luka 5:4-5. Dhana iliyopo ni kwamba muda wa usiku ndio muda wa kuvua samaki. Hili ni jambo ambalo Petro, ambaye ni mtaalam aliyefundishwa, alikuwa analifahamu. Kwa kuongezea, inaonekana walikuwa wameshasafisha vyombo vyao vilivyotumika siku hiyo kwa ajili ya uvuvi katika kipindi kinachofuatia. Unadhani Petro aliuchukuliaje ushauri wa Yesu, kwamba washushe nyavu zao wakati wa mchana? (Tayari Yesu alikuwa na wazo lenye “mwelekeo wa ufundishaji” lililoonesha kuwa ana asili ya useremala (Marko 6:3), sio uvuvi. Sasa, Yesu anapendekeza jambo jingine lifanyike ambalo halioneshi kuwa na uhalisia.)
- Kwa nini Petro anatenda jambo lisilotekelezeka? (Kwa kumheshimu Yesu - na sio uelewa wa Yesu kuhusu masuala ya uvuvi.)
- Soma Luka 5:6-7. Nini kimetokea? (Muujiza. Nyavu zinatengenezwa kwa viwango vya kuvua samaki wa ukubwa na aina mbalimbali. Tukio hili ni zaidi ya matukio ya kawaida!)
- Soma Luka 5:8-9. Unadhani kitu gani kinaendelea akilini mwa Petro kiasi cha kusema maneno haya? (Kwanza, lazima Petro analiangalia jambo hili kama muujiza. Ni matokeo ya nguvu isiyo ya kawaida. Pili, nadhani Petro alikuwa akifikiria kwamba Yesu hana uzoefu na haya masuala ya mitumbwi na uvuvi. Hali hii inamfanya Petro ajisikie hatia.)
- Soma Luka 5:10. Soma tena Luka 5:8. Kauli ya Yesu, “usiogope,” inaongezea jambo gani kwenye ufahamu wetu juu ya kile kinachoendelea mawazoni mwa Petro? (Zaidi ya kujisikia hatia, Petro ana hofu kubwa.)
- “Hofu” inaonekana kuwa hisia ya ajabu dhidi ya mtu ambaye alikuwa amekaa tu kwenye mtumbwi (chomboni) akifundisha habari za Mungu. Unaelezeaje jambo hili? (Jambo pekee linaloleta mantiki kwangu ni kwamba Petro anahitimisha kuwa Yesu ni Mungu. Yesu ni Masihi.)
- Kisa hiki kinatufundisha nini kuhusu kazi yetu na imani yetu?
- Soma Luka 5:11. Soma Mathayo 4:18-20. Huu ni wito wa awali kutoka kwa Yesu. Tunaielewaje kauli “wakaacha vyote wakamfuata?” Je, waliitelekeza kazi yao? (Soma Yohana 21:1-4. Hii inaashiria kuwa hata baada ya mateso na ufufuo wa Yesu bado Yesu anafanya kazi ya uvuvi ili kumwingizia kipato. Marko 1:19-20, Luka 5:8-10 na Mathayo 4:21 zinaashiria kuwa hii ni shughuli ya kifamilia na marafiki. Wanafunzi wanaweza kuacha shughuli yao bila kutelekeza rasilimali za uvuvi. Kimsingi, baada ya wito wa mwisho wa Yesu wanafunzi wanaonekana kufanya kazi muda wote kuitangaza na kuiendeleza injili.)
- Soma Matendo 18:2-4, Matendo 20:33-34 na Matendo 22:2-3. Paulo alikuwa anajitafutia kipato kwa njia gani? (Alikuwa fundi wa kushona hema.)
- Paulo ana elimu ya aina gani? Je, ni sawa na ile ya Petro? (Elimu yake haifanani hata kidogo na ile ya Petro. Paulo ana elimu ya teolojia, hivyo ni mwanateolojia. Pamoja na hayo, anatengeneza mahema ili kujiingizia kipato.)
- Mjadala huu wa Petro na Paulo unatufundisha nini kuhusu asili ya jibu la Petro juu ya wito wa kumfuata Yesu? (Wito wa kumfuata Yesu si lazima umaanishe kwamba tunaachana na utaalam wetu. Ukweli kwamba Yesu alitenda muujiza katika uvuvi wa Petro unaonesha kuwa Yesu alimstawisha katika taaluma yake.)
- Unawezaje kuwa “ndugu katika umoja” na Yesu akiwa ndani ya taaluma yako?
- Dhoruba
- Soma Mathayo 8:23-25. Nani anayepaswa kuwa mtaalamu wa kushughulika na chombo (mtumwi/mashua)? (Wanafunzi waliokuwa wavuvi, na sio Seremala.)
- Hii inatufundisha nini kuhusu kuwa wanafunzi na kufanya kazi kwa kutumia taaluma yetu? (Kwamba tunatakiwa kumtegemea Mungu. Utaalam wetu na uanafunzi wetu sio vitu viwili vinavyotofautiana.)
- Soma Mathayo 8:26. Ungemjibuje Yesu? (Ninaogopa kwa sababu ningeweza kuzama!)
- Kwa nini Yesu anaikosoa imani yao? (Suala kuu maishani mwetu linaangalia kama tunamtumaini Mungu. Yesu anawaambia kuwa ilimradi yu pamoja nao, hawana haja ya kuhofia kifo.)
- Soma Mathayo 8:27. Je, Petro alipaswa kushangaa? (Unaweza kudhani kuwa lile tukio la ajabu la kuvua samaki wengi haukuwa muujiza wa kutosha. Lakini, huu ni muujiza wa wazi kabisa.)
- Hii inatufundisha nini kuhusu ushirika wetu na Mungu? (Tunapaswa kutarajia miujiza. Yesu anadhibiti samaki, pepo na mawimbi. Mvuvi anahitaji nini zaidi? Ikiwa Yesu anadhibiti vipengele vyote vya taaluma yako, unahitaji nini cha ziada? Tunatakiwa kuachana na woga.)
- Soma Mathayo 8:23-25. Nani anayepaswa kuwa mtaalamu wa kushughulika na chombo (mtumwi/mashua)? (Wanafunzi waliokuwa wavuvi, na sio Seremala.)
- Kupandishwa Cheo
- Soma Mathayo 19:27. Petro anasema wameacha kila kitu ili kumfuata Yesu, ingawa hatuna uhakika kabisa juu ya kinachomaanishwa hadi kufikia hapa. Je, Petro anataka nini?
- Soma Mathayo 19:28. Wanafunzi watapokea nini?
- Soma Mathayo 20:20-21 na Marko 10:35-37. Hii inafuatia baada ya mjadala wa Yesu kuhusu kiti cha enzi na kuyahukumu makabila. Je, hapa “mkuu” inamaanisha nini? (Ukuu katika ufalme wa Yesu.)
- Soma Marko 9:33-35. Hii inatufundisha nini kuhusu kung’ang’ania kupandishwa cheo kazini? (Uongozi wa kuwatumikia watu wengine. Ikiwa unataka kupandishwa cheo, unatakiwa kuwa radhi kuwatumikia watu wote. Unatakiwa kuwa radhi kufanya kazi ngumu.)
- Soma Marko 9:36-37. Hili linaonekana kuwa jambo la ajabu kidogo. Kwa nini mtu mzima asimkaribishe mtoto? Mtu mzima ana mambo mengi ya msingi anayotakiwa kuyafanya. Ikiwa unataka kupandishwa cheo na kupata mamlaka, mtoto hana mamlaka ya kugawiana na watu.)
- Unadhani Yesu anamaanisha nini kuhusu kupandishwa cheo? (Ikiwa unataka kupandishwa cheo, unatakiwa kuwa radhi kufanya “kazi ya kuwatumikia wengine” na unatakiwa “kuwakaribisha” wale ambao hawawezi kukutendea mema.)
- Ngoja nikuulize swali linalohusiana na hili. Je, unafahamu jina la mtu anayesafisha ofisi yako? Unawatendeaje watu unaowaongoza? Unawatendeaje wafanyakazi wenzako ambao hawana uwezo wa kukupandisha cheo?
- Soma Mathayo 20:17-19. Endapo ungekuwa unasikiliza maelezo haya, je, ni ya dhati kwa kiasi gani?
- Soma Mathayo 20:20-22. Je, unadhani wanafunzi hawa (Yakobo na Yohana) walikuwa wanasikiliza kwa makini kile ambacho Yesu amekisema?
- Kama hawakuwa makini, ni kwa nini? (Sidhani kama walikuwa makini, na ni kwa sababu walikuwa wanajizingatia wao wenyewe.)
- Ikiwa hawakuwa makini kuhusu suala la kuteswa kwake, je, walielewa makubaliano yao kunywea “kikombe nitakachonywea mimi?”
- Hii inatufundisha nini kuhusu kupandishwa cheo? (Walikuwa wanajizingatia wao wenyewe, na sio kwenye masuala yanayohusu ustawi wa Yesu. Hii ni sehemu moja ya taswira pana ambayo Yesu anaizungumzia kuhusu uongozi. Ikiwa unataka kuongoza, hutakiwi kuwa mbinafsi na kuwakaribisha wale wasioweza kukusaidia. Ikiwa unataka kuongoza, unatakiwa kuzingatia mahitaji ya watu wengine, na sio kujikita kwenye mahitaji yako mwenyewe.)
- Kama hawakuwa makini, ni kwa nini? (Sidhani kama walikuwa makini, na ni kwa sababu walikuwa wanajizingatia wao wenyewe.)
- Rafiki, je, uko radhi kufungamanisha imani yako na kazi yako? Sidhani kama hiki zaidi kinahusu kuwaambia watu habari za Yesu wakati ambapo hawataki kusikiliza. Nadhani inahusiana na kutumia kanuni za Biblia unapofanya kazi yako. Kanuni hizi zimejengwa juu ya Mungu, kumtumaini Mungu kutatua matatizo yetu, kuwa radhi kufanya kazi ambazo watu wengine hawataki kuzifanya, kuwakaribisha wafanyakazi wenzako ambao hawana uwezo wa kukupandisha cheo, na kuyazingatia mahitaji ya watu wanaokuzunguka badala ya wewe kuyazingatia mambo yako wewe mwenyewe. Je, utajitoa kufuata hizi kanuni za upandishaji vyeo?
- Juma lijalo: Pambano Kuu na Kanisa la Awali.